Na Cresencia Kapinga, JamhuriMedia, Ruvuma

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Ruvuma imewafikisha mahakamani watu wawili kwa tuhuma za kukiuka sheria za ushuru wa bidhaa na kufanya uzalishaji wa pombe kali bila kibali halali.

Akizungumza na waandishi wa Habari Jana ofisini kwake Meneja wa TRA Mkoa wa Ruvuma Nicodemus Mwakilembe alisema kuwa washtakiwa hao Khadija Hiza na Abraham Mosile wanadaiwa kubandika stika za ushuru wa bidhaa na kuzalisha pombe bila kuwa na leseni kutoka kwa Kamishna wa Kodi za ndani kinyume na taratibu za Sheria za Kodi nchini.

Alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya operesheni zinazoendelea za kudhibiti vitendo vya ukwepaji kodi na kulinda mapato ya serikali na si vinginevyo.

Mwakilembe amesema kuwa mamlaka itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watu au makampuni yanayojihusisha na uzalishaji au usambazaji wa bidhaa bila kufuata sheria.

Kwa upande Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka TRA, Medalakini Emanuel, amesema kesi hiyo imesomwa katika Mahakama ya wilaya ya Songea chini ya hakimu mkazi mwandamizi Christina Haule ambapo watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na bidhaa za pombe kali aina ya La Chalz Beverages Lion Spirit ambazo zilipaswa kulipiwa ushuru wa bidhaa lakini zilikutwa zikiwa na stempu za kielektroniki bandia.

Wakili Emmanuel alisema kuwa kati ya makosa nane yanayowakabili watuhumiwa hao, matatu ni ya kukutwa na bidhaa zilizopaswa kulipiwa ushuru wa bidhaa zikiwa na stempu bandia, huku makosa mengine yakihusisha kukwepa kodi kwa udanganyifu wa kubandika stempu zisizo halali.

Aidha, kosa la nane ni la uhujumu uchumi, ambapo watuhumiwa wanadaiwa kuisababishia TRA hasara kutokana na kitendo cha kukwepa kulipa kodi stahiki.

Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea kusikilizwa katika mahakama ya Wilaya , huku washtakiwa wakisubiri hatua zaidi za kisheria zitakazofuata.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Ruvuma Nicodemus Mwakilembe