Na Cresencia Kapinga, JamhuriMedia, Ruvuma
Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma linawashikilia watu watatu katika matukio mawili tofauti, likiwemo la mwendesha bodaboda kuporwa pikipiki na kisha kuuwawa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 2, 2026 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Marco Chilya aliwataja watuhumiwa kuwa ni Said Ramadhani (28) Mkazi wa Mshangano eneo la Namanyigu Manispaa ya Songea, Gamaliel Mundo (38) Mkazi wa eneo la Mtyangimbole katika halmashauri ya Madaba na Michael Ngonyani (38) Mkazi wa Mtyangimbole Madaba.
Kamanda Chilya alifafanuwa zaidi kuwa mnamo Machi 18 mwaka huu Majira ya Usiku watuhumiwa wawili ambao ni Said Ramadhani na Gamaliel Mundo inadaiwa kuwa walimteka mwendesha bodaboda Lukas Msongela (32) Mkazi wa Mkuzo Manispaa ya Songea na kumpeleka eneo la Peramiho nje kidogo ya mji wa Songea kisha walimshambulia kwa kutumia kitu butu na kumsababishia kifo chake.
Alisema kuwa baada ya kutokea tukio hilo Jeshi la Polisi mkoani humo kwa kutumia timu ya wataalam wakufwatilia matukio makubwa ilianza ufuatiliaji wa haraka na ilipofika Machi 27, mwaka huu, huko katika Kijiji Cha Mtyangimbole polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wote wawili wakiwa wamejificha .
Aliongeza kuwa hata hivyo baada ya ufwatiliaji Polisi walibaini kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakijihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwa ni pamoja na uvunjaji na wizi wa pikipiki wilayani Songea.
Kamanda Chilya alisema kuwa upelelezi wa tukio hilo unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa Mahakamani kujibu mashaka yanayowakabili.
Aidha katika tukio lingine kutokana na operesheni na misako inayoendelea mkoani Ruvuma mnamo Machi 31 mwaka huu polisi pia walifanikisha kumkamata Michael Ngonyani Mkazi wa Mtyangimbole ambaye anadaiwa alikuwa akijihusisha na uhalifu wa aina nyingi ikiwa ni pamoja na wizi wa magari mkoani Mbeya na baada ya kupekuliwa na mahali alipokuwa akiishi alikutwa akiwa na vitu mbalimbali ambayo vinadhaniwa kuwa ni vya wizi.
Kamanda Chilya alivitaja vitu vinavyodhaniwa kuwa ni vya wizi alivyokamatwa navyo kuwa ni Gari aina ya Toyota IST yenye namba za kusajiri T.829 DYH,Leseni nne za udereva zenye majina ya watu tofauti tofauti , Sound bar Moja aina ya sky wood, luninga mbili za inchi 65 na 55 pamoja na water pump Moja..
Alitaja vitu vingine mtuhumiwa alivyokamatwa navyo alikutwa akiwa na sare za jeshi la Polisi (kaki) Jozi Moja na sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) suruari moja na T shert moja ambazo anadaiwa alikuwa anazitumia maeneo mbalimbali kwa kujifanya askari wa majeshi hayo na kwamba mtuhumiwa huyo anatarajia kufikishwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.





