Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza
Watengeneza maudhui nchini wamehamasishwa kutumia ubunifu wao kujipatia kipato kupitia fursa zitokanazo na nishati safi ya kupikia, kwa kuelimisha jamii kupitia kazi zao zikiwemo video za elimu, vichekesho, hadithi na kampeni mbalimbali zitakazowafikia wananchi kwa urahisi.
Wito huo umetolewa Aprili 1, 2026 jijini Mwanza na Mhandisi Nishati kutoka Wizara ya Nishati, Benezeth Kabunduguru, wakati akizungumza katika mafunzo kwa watengeneza maudhui (content creators).
Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, huku Wizara ya Nishati ikiwa miongoni mwa wawezeshaji wakuu.
Amesema mafunzo hayo yamelenga kuwasaidia watengeneza maudhui kuboresha kazi zao kwa kuzingatia mbinu za kubiasharisha maudhui mtandaoni, kujenga chapa binafsi pamoja na kuzingatia masuala ya hakimiliki.
Kabunduguru ameeleza kuwa watengeneza maudhui wana nafasi kubwa ya kubadilisha mtazamo wa jamii kupitia ubunifu wao, akisisitiza kuwa maudhui yenye ubora na mvuto yanaweza kununuliwa na kuwapatia kipato waandaaji wake, sambamba na kusambaza ujumbe muhimu kwa jamii.
Aidha, amesema Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Amebainisha kuwa suluhisho za nishati hiyo tayari zipo na zinaendelea kuwafikia wananchi, huku changamoto kubwa ikiwa ni upatikanaji wa taarifa sahihi kwa watu wengi zaidi.
Kutokana na hali hiyo, amewataka watengeneza maudhui kuchangamkia fursa hiyo kwa kuandaa kazi zitakazolenga kuelimisha kuhusu faida za nishati safi ya kupikia na madhara ya matumizi ya nishati zisizo safi.
Amesisitiza kuwa utoaji wa taarifa sahihi kwa jamii utachochea mabadiliko chanya yatakayoboresha maisha ya wananchi na kulinda afya za Watanzania.









