Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Leo naandika makala hii saa chache kabla ya kwenda kanisani kumwabudu na kumsujudia Bwana wetu Yesu Kristu Mfufuka. Ninao wajibu kwangu, kwa familia, kwa Kanisa, kwa taifa na kwa ndugu, jamaa na marafiki bila kujali imani yao. Nawapongeza ndugu zetu Waislamu kwa mfungo mtukufu walioumaliza yapata siku 11 zilizopita.

Mfungo wa mwaka huu umekuwa baraka kwa imani zetu sote. Tumeanza pamoja, tumehitimisha kwa nyakati tofauti. Ndugu zetu Waislamu, kwa kufuata kitabu kitakatifu, wamehitimisha mfungo wa siku 30 kama nilivyoainisha.

Sisi Wakristo, tumehitimisha mfungo wa siku 40, Dominika—au siku mbili zilizopita kwa maana ya Jumapili iliyopita. Sisi Wakatoliki tunatumia neno Dominika badala ya Jumapili.

Nafahamu watu wanajiuliza, inakuwaje Dominika iliyopita zilikuwa siku 46. Sisi Wakatoliki tunafunga Jumatatu hadi Jumamosi. Tulianza mfungo Jumatano ya Majivu, Februari 18, 2026.

Sitanii, mimi nikiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia ya Roho Mtakatifu Kitunda, namshukuru sana Paroko wangu, Baba Stefano Kaombe, ambaye ni mwema na si mbaguzi wa imani.

Baba Paroko Kaombe muda wote anahubiri upendo, undugu na maendeleo ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla. Namshukuru sana. Lakini pia, katika dhana ya shukurani, namshukuru Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa tukio la kihistoria.

Kabla ya Pasaka, zilizagaa taarifa kuwa Rais Trump amekataa kuwalipa dola milioni 50 msaidizi wa aliyekuwa Rais wa Venezuela, Nicolaus Maduro, na walinzi wawili waliomuuza Januari 3, 2026, na hatimaye akakamatwa.

Marekani ilitoa ahadi ya kulipa dola milioni 50 kwa mtu ambaye angemsaliti Rais wa Venezuela, Maduro. Huu ni mwendelezo wa mvutano wa kisiasa nchini humo. Kiongozi wa upinzani, Maria Corina Machado, alidhani akiondoka Maduro, basi yeye angekuwa Rais.

Trump akamwambia kuwa si “presidential material.” Sina uhakika kama viongozi wetu wa kisiasa wana kitu cha kujifunza!

Sitanii—nataka hili liwe fundisho kwa wasaliti wa Afrika, Amerika Kusini na Asia, wanaodhani Wazungu wanaipenda sana Afrika. Hawa wana malengo binafsi. Afrika tushikamane. Wapinzani wanazo hoja nyingi wanazoweza kuzitumia kuingia madarakani bila kuchoma nchi zao.

Wazungumze jinsi ya kumaliza matatizo ya nchi zetu—ikiwamo afya, maji, elimu na miundombinu. Yapo mengi ya kuwafanya wananchi wawaamini na kuwapa madaraka, lakini wao wanakimbia kushitaki na kuuza viongozi wa nchi zao. Sasa angalia alichowafanya Trump huko Venezuela. Safi sana, Trump.

Katika kufufuka kwake Yesu, ninayo mawazo. Unaweza usikubaliane na mimi, lakini yaangalie. Siku hizi, kelele zimekuwa nyingi kuliko hata sauti ya dhamiri. Kila mmoja ana lake—wapo wanaotafuta madaraka, wapo wanaotafuta umaarufu, na wapo wanaotafuta kujaza matumbo yao. Lakini katika pilikapilika hizi zote, kuna somo kubwa tunalisahau: ufufuko wa Yesu Kristo.

Ufufuko si tukio la kidini tu; ni alama ya ushindi wa mema dhidi ya mabaya, matumaini dhidi ya kukata tamaa, na umoja dhidi ya mgawanyiko. Ni ujumbe kwamba hata pale ambapo mambo yanaonekana kufa—umoja wetu, mshikamano wetu, hata ndoto zetu za taifa—bado kuna nafasi ya kufufuka tena.

Leo hii, tukizungumzia Tanzania, hatuhitaji darubini kuona nyufa zinazotugawa. Kuna tofauti za kisiasa, kiuchumi na hata kijamii. Watu wanatazamana kwa shaka, wengine wakiona wenzao si washirika tena bali wapinzani. Lakini je, huu ndio urithi tunaoutaka tunapoelekea katika dira ya mwaka 2050?

Dira ya 2050 si karatasi ya kuweka kwenye makabati ya ofisi; ni ahadi ya pamoja ya taifa. Ni ndoto ya kuona Tanzania yenye uchumi imara, jamii yenye haki na wananchi wenye ustawi. Lakini ndoto hii haiwezi kujengwa juu ya msingi wa chuki, ubinafsi na kukosa mshikamano. Inahitaji moyo ule ule uliodhihirishwa katika ufufuko—moyo wa kusamehe, kushirikiana na kuanza upya.

Tukiangalia mfano wa ufufuko, tunaona jambo moja muhimu: baada ya mateso na kifo, kulikuwa na mwanzo mpya. Hii inatufundisha kuwa hata pale tulipokosea kama taifa, hata pale tulipogawanyika, bado tuna nafasi ya kurekebisha na kusonga mbele kwa pamoja. Swali la kujiuliza ni hili: je, tuna utayari huo?

Wanasiasa wetu wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kujenga umoja huu. Siasa isiwe chanzo cha uhasama, bali iwe daraja la kuunganisha mawazo tofauti kwa manufaa ya taifa. Lakini pia, wananchi hatupaswi kubaki watazamaji. Umoja unaanzia kwa mtu mmoja mmoja—jinsi tunavyoongea, tunavyoheshimu tofauti na tunavyoweka maslahi ya taifa mbele ya maslahi binafsi.

Tusidanganywe; maendeleo si majengo marefu wala takwimu nzuri za uchumi pekee. Maendeleo ya kweli yanatokana na jamii iliyo imara, yenye mshikamano na inayojali. Bila hilo, hata mipango mizuri zaidi itabaki kuwa ndoto zisizotekelezeka.

Katika kipindi hiki cha kukumbuka ufufuko, tujiulize: tunafufua nini kama taifa? Je, tunafufua matumaini au tunazika umoja wetu? Je, tunajenga au tunabomoa? Kila mmoja ana nafasi ya kuchagua upande.

Ni wakati wa kuacha siasa za migawanyiko na kuanza siasa za maendeleo. Ni wakati wa kuacha lawama na kuanza uwajibikaji. Ni wakati wa kuacha ubinafsi na kuanza kujenga Tanzania ya pamoja. Hii ndiyo roho ya ufufuko tunayopaswa kuibeba.

Tukifanya hivyo, dira ya 2050 haitakuwa ndoto ya mbali bali uhalisia unaogusika. Tutakuwa taifa linalosimama imara si kwa sababu ya rasilimali zake pekee, bali kwa sababu ya umoja wa watu wake. Na hapo ndipo tutakapothibitisha kwamba tumeelewa maana halisi ya ufufuko—si kwa maneno, bali kwa matendo.

Mungu ni mwema.

0784 404 827