Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, ameagiza Tume ya Madini kuboresha mfumo wa utoaji wa leseni za madini ili kuongeza ufanisi, kuimarisha uwazi na kupunguza migogoro katika shughuli za utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini nchini.

Mbibo ametoa maelekezo hayo leo, Julai 5, 2026, alipotembelea banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Amesema utoaji wa leseni kwa wakati na kwa kuzingatia taratibu utaongeza imani ya wadau, kuimarisha utendaji wa sekta na kujenga heshima ya Wizara ya Madini pamoja na sekta ya madini kwa ujumla.

“Tutengeneze sekta inayoheshimiwa. Jinsi mtakavyofanya vizuri, ndivyo mtakavyozidi kujenga heshima ya sekta ya madini na Wizara kwa ujumla,” amesema.

Mbali na hilo, Mbibo ameipongeza Tume ya Madini kwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato, akisema mafanikio hayo ni kielelezo cha usimamizi mzuri wa rasilimali za madini na mchango wake unaozidi kuimarika katika uchumi wa Taifa.

“Hongereni kwa kuvuka lengo la makusanyo, mmefanya vizuri. Madini yana thamani kubwa kwa Taifa, hivyo tunapaswa kuongeza bidii ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa nchi,” amesema.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu shughuli za madini ili kuondoa dhana potofu zinazohusisha uchimbaji wa madini na imani za kishirikina.

Ameeleza kuwa mafanikio katika sekta ya madini yanatokana na elimu, utafiti wa kijiolojia, matumizi ya teknolojia na uwekezaji, hivyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kutachochea ushiriki wao katika kunufaika na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.