-Wasema unaongeza uwazi, ufanisi na kuokoa muda wa kupata huduma
Na Grace Michael, Dar es Salaam
Wananchi na wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wamepongeza Mfumo wa Kujihudumia Binafsi (Self Service) unaowezesha wanachama kupata huduma mbalimbali kupitia simu janja, wakisema mfumo huo umeongeza uwazi katika utoaji wa huduma, kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuokoa muda ambao awali walilazimika kuutumia kufika katika ofisi za NHIF.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walipotembelea banda la NHIF katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, wananchi hao walisema maboresho ya mifumo ya kidijitali ya NHIF yameongeza ufanisi na kuimarisha usimamizi wa huduma za bima ya afya.
Bw. Emmanuel Selemani alisema mfumo huo unampa mwanachama uwezo wa kuona historia ya huduma zote alizopata katika vituo vya kutolea huduma za afya, hatua inayochangia kuongeza uwazi na kuwapa wanachama nafasi ya kushiriki katika kulinda rasilimali za Mfuko.
“Mfumo huu ni mzuri sana kwa sababu kila mwanachama anaweza kuona huduma alizopata katika kituo cha afya. Ikitokea kuna huduma zimeonekana kwenye mfumo lakini hakuzipata, anaweza kutoa taarifa NHIF ili zifuatiliwe. Hii itasaidia kudhibiti na kuzuia vitendo vya udanganyifu katika utoaji wa huduma,” alisema.
Kwa upande wake, Bi. Maria Nzalima alisema ameridhishwa na huduma zinazotolewa katika banda la NHIF kwenye maonesho hayo kutokana na kasi ya utoaji wa huduma pamoja na elimu aliyopata kuhusu haki na wajibu wa mwanachama wa NHIF.
“Huduma ni za haraka na nimepata elimu muhimu kuhusu namna ya kutumia bima yangu pamoja na haki na wajibu wangu kama mwanachama. Hii imeniongezea uelewa na kujiamini ninapotumia huduma za NHIF,” alisema.
Akizungumza kuhusu huduma zinazotolewa katika banda la NHIF, Ofisa Uanachama Mwandamizi, Bw. Hassan Ally, alisema wananchi wanapata huduma mbalimbali ikiwemo usajili kupitia vifurushi mbalimbali vya bima ya afya, elimu ya matumizi ya Mfumo wa Self Service, uhuishaji wa taarifa za wanachama, kubadilisha namba za simu pamoja na kuunganisha taarifa zao na Mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Aliongeza kuwa maonesho hayo yanatoa fursa muhimu kwa wananchi kupata elimu kuhusu huduma za NHIF na kujisajili ili waweze kunufaika na huduma za bima ya afya.
“Tunawahamasisha wananchi wote kutembelea banda la NHIF lililopo ndani ya Banda la Kijiji cha Bima ili kupata elimu, kujisajili na kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na Mfuko kwa wanachama wake,” alisema.
NHIF imeendelea kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam kila mwaka ikiwa ni sehemu ya jitihada za kusogeza huduma kwa wananchi, kutoa elimu kuhusu bima ya afya na kuhamasisha ushiriki katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.





