Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) amepongeza mafanikio yanayoendelea kupatikana katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), akisema yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza biashara, uwekezaji na uchumi wa Taifa.
Akizungumza leo Julai 10 baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho hayo, Gavana amesema Sabasaba imeendelea kutoa fursa kwa Watanzania kujifunza, kupata huduma mbalimbali na kujionea bidhaa pamoja na teknolojia mpya zinazochochea maendeleo ya kiuchumi.
Amesema maonesho ya mwaka huu, yanayoadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, yamevutia ushiriki wa mataifa zaidi ya 25, hali inayoonesha hadhi yake ya kimataifa na mchango wake katika kukuza biashara za ndani na nje ya nchi.
Akizungumzia sera ya fedha, Gavana amesema uamuzi wa Benki Kuu kuweka kiwango cha riba cha asilimia 6.25 umefanyika kwa kuzingatia hali ya uchumi na lengo la kuhakikisha utulivu wa bei pamoja na kuimarisha shughuli za uzalishaji.
Ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha ukwasi wa kutosha katika mabenki ya biashara ili yaendelee kutoa mikopo kwa sekta binafsi na wakati huo huo kudhibiti mfumuko wa bei ubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5.
Aidha, amesema kuanza kwa msimu wa mavuno kunatarajiwa kuimarisha thamani ya shilingi ya Tanzania, hali itakayowawezesha wakulima kupata bei nzuri ya mazao yao na kuongeza manufaa kwa wafanyabiashara wanaouza bidhaa katika masoko ya nje.
Katika hatua nyingine, Gavana amesema Benki Kuu ipo katika hatua za mwisho za kuandaa mfumo wa kisheria utakaosimamia matumizi ya sarafu za kidijitali na mali za mtandao (virtual assets), ikiwemo Bitcoin na stablecoins.
Amesema tayari Benki Kuu imeandaa waraka wa awali (concept note), pamoja na rasimu ya sheria na kanuni, ambazo zinaendelea kuwasilishwa katika taasisi husika, ikiwemo Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Baraza la Mawaziri na baadaye Bunge kwa hatua za mwisho za kupitishwa.
Gavana amesema uwepo wa sheria hizo ni muhimu ili kukabiliana na vihatarishi vinavyoweza kujitokeza kupitia matumizi ya sarafu za kidijitali, ikiwemo utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na kulinda uwekezaji pamoja na mitaji ya Watanzania.
Kwa upande wa elimu ya fedha, Gavana amesema ameridhishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi wanaotembelea mabanda ya Benki Kuu na Chuo cha Benki Kuu kupata elimu kuhusu huduma za kifedha na usimamizi wa fedha binafsi.
Amesema BOT imeandaa programu maalumu ya elimu ya fedha itakayofanyika mwezi Novemba mwaka huu, ambapo tayari zaidi ya washiriki 200 wamejiandikisha kushiriki mafunzo hayo.


