Na Prosper Makene_

Geneva, Uswisi, Julai 09, 2026 – Tanzania imepewa heshima ya kimataifa baada ya kutunukiwa Tuzo ya WSIS Prizes 2026 kutokana na mafanikio ya mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano. Mradi huo umefanikiwa kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na maeneo ambayo awali hayakuwa na huduma yoyote ya mawasiliano nchini.

Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.) katika hafla iliyofanyika Geneva, Uswisi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Kairuki amesema utambuzi huo ni ushuhuda wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha hakuna Mtanzania anayesahaulika katika upatikanaji wa huduma za kidijitali.

“Tumejipanga kuhakikisha kila kijiji kina mawasiliano. Minara 758 imefungua fursa mpya za biashara, elimu, afya na huduma za serikali kwa wananchi wetu wa vijijini,” alisema Waziri Kairuki.

Mradi huo ulizinduliwa rasmi na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 10 Aprili, 2026.

Aidha, Tanzania ilipata uteuzi katika vipengele saba (7) vya Tuzo za WSIS 2026 na kuibuka na tuzo mbili kwa ujumla. Nchi pia imetunukiwa vyeti vya kutambua miradi mingine iliyofanya vizuri.

Tuzo za WSIS zinatolewa na Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano ITU kutambua miradi inayochangia katika kufikia malengo ya Mkutano wa Dunia kuhusu Jumuiya ya Habari, ikiwemo kupunguza pengo la kidijitali.