Papa Leo XIV amemteua Padre Vincent Lawrence Mpwaji, kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu DSM. Pia amemteua kuwa Askofu wa heshima (Titular Bishop) wa jimbo la Tacarata huko Algeria.

Kwa kawaida Maaskofu wasaidizi (Auxiliary Bishops) hupewa majimbo ya heshima (Titular Diocese) ambayo hayana nafasi za kiutawala za moja kwa moja. “Titular dioceses” ni mjimbo ya zamani ya Kanisa Katoliki ambayo hayana tena waamini au utawala wa moja kwa moja kwa sababu ya mabadiliko ya kihistoria kama vile vita, uhamiaji, mabadiliko ya tamaduni au kupotea kwa jumuiya ya Kikristo.

Askofu Mpwaji alizaliwa tar.5 June 1978, mjini Morogoro. Mwaka 1993 alijiunga na seminari ya Visiga kwa masomo ya sekondari na malezi ya kiroho hadi 1996. Aliendelea na A-level Mazengo sekondari na kuhitimu 1999.

Alijiunga na Seminari Kuu ya Mtakatifu Anthony wa Padua (Ntungamo) na kuhitimu shahada ya kwanza ya Falsafa (Bachelor degree in Philosophy) mwaka 2003. Kisha akaendelea na masomo ya Theolojia (Bachelor degree in Theology) Seminari Kuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga (Segerea) na kuhitimu 2007.

Tar.7 July 2008 alipata Daraja takatifu la Upadre kisha akateuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Idara ya Elimu Jimbo Kuu DSM na baadae Wakili wa Mahakama ya Kanisa, Jimbo Kuu DSM.

Mwaka 2011 alitumwa Chuo Kikuu cha Gregorian, Roma kwa shahada ya umahiri ya Theolojia (Masters degree in Theology) na kuhitimu mwaka 2014. Alirejea na kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Miradi Jimbo Kuu DSM.

Mwaka 2015 alitumwa tena Gregorian University, kwa shahada ya uzamivu ya Theolojia (Doctorate in Dogmatic Theology). Alipaswa kuhitimu mwaka 2020 lakini aka-postpone akimuuguza Hayati Kadinali Pengo. Hatimaye akahitimu mwaka 2021.

Aliporejea alipangiwa Parokia Kuu ya St.Joseph kuwa Paroko Msaidizi na Kansela wa Jimbo Kuu DSM. Askofu Mpwaji anachukua nafasi ya Askofu Stephano Musomba, OSA ambaye aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Bagamoyo March 2025.

Kufuatia uteuzi huu, sasa Jimbo Kuu DSM litakuwa chini ya Askofu Mkuu Yuda Thedeus Ruwaichi, OFM Cap, na Maaskofu wasaidizi wawili, Henry Mchamungu na Vincent Mpwaji. Tumtakie heri Askofu Mpwaji katika utume wake mpya. Roma locuta; causa finita est. Roma ikisema mjadala umefungwa.