Na Eva Ngowi na Chedaiwe Msuya, WF

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Mzenzi, ametembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), na kupongeza jitihada za Wizara hiyo za kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya fedha, uchumi na usimamizi wa rasilimali za umma.

Prof. Mzenzi alisema Banda hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuwaelimisha wananchi kwa kuwa linatoa taarifa na ufafanuzi kuhusu sera, mipango na huduma mbalimbali zinazoratibiwa na Wizara ya Fedha pamoja na taasisi zake, hatua inayochangia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya uchumi wa Taifa.

Alisema uwepo wa wataalamu kutoka Wizara ya Fedha katika Maonesho hayo unawapa wananchi fursa ya kuzungumza moja kwa moja na wabobezi, kuuliza maswali na kupata majibu sahihi kuhusu huduma za kifedha na maendeleo ya sekta ya fedha nchini.

Aidha, Prof. Mzenzi alieleza kuwa utoaji wa elimu kupitia Maonesho ya Sabasaba unaimarisha uwazi, huongeza ushiriki wa wananchi katika masuala ya maendeleo na kuhamasisha matumizi ya huduma rasmi za kifedha, jambo linalochochea ukuaji wa uchumi jumuishi.

Kwa upande wao, wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha walieleza kuridhishwa na huduma za elimu na ushauri walizopatiwa, wakisema zimewaongezea uelewa kuhusu masuala ya fedha, uchumi na huduma mbalimbali zinazotolewa na Wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake.

Mmoja wa wananchi hao, Bi. Fatuma Mshana, alisema maelezo aliyopata kutoka kwa wataalamu wa Wizara ya Fedha yamemsaidia kuelewa kwa kina zaidi masuala ya fedha na umuhimu wa kufuatilia taarifa rasmi zinazotolewa na Serikali.

Aliongeza kuwa amevutiwa na namna watumishi wa Wizara ya Fedha walivyokuwa wakitoa huduma kwa weledi, uwazi na heshima kwa wananchi, akibainisha kuwa elimu hiyo itamsaidia kufanya maamuzi bora zaidi kuhusu masuala ya kifedha.

Banda la Wizara ya Fedha limeendelea kuvutia idadi kubwa ya wananchi wanaotembelea Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Wizara na taasisi zake, huku wengi wakiondoka wakieleza kuridhishwa na kiwango cha huduma na elimu waliyoipata.