Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema sababu ya msingi ya kutekeleza kwa gharama kubwa katika bandari ya Dar es Salaam ni huduma bora kwa wateja wa bandari.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA’ Bw Plasduce Mbossa, serikali inagharamia miradi mikubwa bandarini kwa sababu inataka bandari yetu iwe ya kisasa, ifanye kazi kwa ufanisi na itoe huduma shindani duniani. “Lengo ni kujiridhisha kwamba bandari yetu inafanya kazi kwa ufanisi, inatoa huduma shindani na bora kwa wateja wetu.”
Bw Mbossa alisema kaulimbiu ya Wiki ya Huduma kwa Wateja ya “Hatua ya Ziada” itakuwa mwongozo wa utendaji wa Mamlaka katika kuhakikisha wateja wanapata huduma bora na bidhaa zao zinahudumiwa na kutolewa kwa wakati.
Mkurugenzi Mkuu huyo amefafanua kuwa mamlaka imeweka mkazo katika kuboresha huduma kwa wateja na kuongeza uwezo wa bandari zake kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu, huku ikilenga kuhakikisha wafanyabiashara wanachukua mizigo yao kwa wakati.
Mbossa alisema mafanikio ya TPA yanaonekana ndani ya nchi na kimataifa, akibainisha kuwa Bandari ya Dar es Salaam imepanda kutoka nafasi ya 360 na kufikia nafasi 255 katika viwango vya ubora duniani. “Haya ni matokeo ya uwekezaji unaolenga maboresho ambao umefanywa na TPA inaendelea kutekeleza miradi ya kuongeza uwezo wa kuhudumia meli na mizigo.”
Ameishukuru Serikali kwa kuiruhusu TPA kukopa dola milloni 500 za Marekani kwa ajili ya kuendelea kuboresha bandari nchini.Miongoni mwa miradi inayoendelea ni ujenzi wa matanki 15 ya kuhifadhi mafuta katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam, ambao umefikia asilimia 52 ya utekelezaji.
Mbossa alisema miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa Bandari Kavu ya Kurasini na upanuzi wa Bandari ya Mtwara, unaolenga kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena kama saruji, makaa ya mawe na bidhaa nyingine zinazofanana.
“Pamoja na maboresho hayo, tunafanya pia ujenzi wa Gati la Malindi lililopo hapa Dar es Salaam, mbele ya Makao Makuu ya Mamlaka,” alisema.
Kwa upande wa Bandari ya Dar es Salaam, Mbossa alisema TPA ina mpango wa kuboresha zaidi bandari ya Dar es Salaam kwa kujenga Gati Namba 12 hadi 15 na kuimarisha Gati Namba 8 hadi 11, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia meli na mizigo kwa ufanisi zaidi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, Balozi Ernest Mangu, amepongeza Bandari ya Dar es Salaam kwa utendaji mzuri unaodhihirika hivi sasa na kuwaomba wadau wa usafirishaji wa mizigo kuhakikisha wanachukua mizigo yao kwa wakati ili kupunguza msongamano bandarini.
Balozi Ernest Mangu, ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) mstaafu, amewataka wafanyakazi kufanyakakazi kwa ufanisi ili kuendelea kuimarisha imani ya watumiaji wa huduma za bandari.
“Ongezeko la mizigo limeibua changamoto nyingine, ikiwamo msongamano wa malori katika barabara zinazoelekea bandarini na katika vituo maalumu vya kuhifadhia na kusafirishia mizigo (ICDs),” alisema Balozi Mangu.
Aliitaka TPA, kampuni za usafirishaji wa mizigo na wadau wengine katika sekta hiyo kushirikiana kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo, ili kuhakikisha ongezeko la shughuli za bandari haliathiri ufanisi wa huduma kwingineko.
Balozi Mangu alisema TPA inapaswa kutumia ubunifu na kubaini mapungufu ya kiutendaji ndani ya taasisi hiyo badala ya kutegemea zaidi kutafuta wateja wapya, akisisitiza kuwa ufanisi wa huduma ndiyo msingi wa kuvutia na kuwahifadhi wateja katika soko lenye ushindani mkubwa.
“Lengo letu ni kuhakikisha bandari zinaendelea kuwa kiungo muhimu katika kukuza uchumi na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Sekta ya umma inahitaji kushirikiana na sekta binafsi katika kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050,” alisema.
Katika hafla hiyo, Balozi Mangu pia alitoa tuzo kwa wafanyakazi 12 waliofanyakazi vizuri kutoka idara mbalimbali za TPA, huku akiwataka kuendelea kuongeza bidii na ubunifu ili kudumisha kiwango cha utendaji na kuwa mfano kwa watumishi wengine.
Aidha, aliwataka Watanzania kujivunia uwepo wa Bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine nchini na kuzitumia kusafirisha bidhaa mbalimbali, hususan mazao ya kilimo kama nafaka, matunda na mbogamboga, ili kuongeza fursa za biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi.




