Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki kikamilifu katika Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), unaofanyika tarehe 6 hadi 9 Oktoba 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, Tanzania.
Mkutano huo unaofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 40 ya Mkataba wa Nairobi umebeba kaulimbiu “Towards Sustainable Blue Economy in the Western Indian Ocean Region for People and Nature: A Journey of Forty Years.”
Ushiriki wa NEMC unaakisi jukumu lake la kisheria na kitaalamu katika usimamizi na uhifadhi wa mazingira, ikiwemo udhibiti wa uchafuzi, tathmini ya athari za kimazingira, uzingatiaji wa viwango vya mazingira na ulinzi wa mifumo ikolojia ya bahari na pwani.
Kupitia COP12, NEMC inawakilisha masuala ya mazingira ya Tanzania katika majadiliano ya kikanda kuhusu uchafuzi wa bahari, mabadiliko ya tabianchi, uhifadhi wa bioanuai na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.
Aidha, NEMC inatumia jukwaa hilo kuimarisha ushirikiano na taasisi za kitaifa, kikanda na kimataifa kwa kubadilishana uzoefu, utaalamu na teknolojia katika usimamizi wa mazingira.
Ushirikiano huo ni muhimu katika kuunganisha utekelezaji wa majukumu ya kitaifa na ahadi za kimataifa za Tanzania katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu.
COP12 pia inatoa fursa kwa NEMC kutafuta na kuimarisha fursa za ufadhili, uwekezaji na ushirikiano katika miradi ya mazingira, ikiwemo uhifadhi wa bioanuai, tafiti, udhibiti wa uchafuzi, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuendeleza Uchumi wa Buluu.
Jukwaa hili pia linawezesha NEMC kutangaza uzoefu na mchango wa Tanzania katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira.
Kwa ujumla, ushiriki wa NEMC katika COP12 unaimarisha nafasi ya Tanzania katika agenda ya uhifadhi wa mazingira ya bahari na pwani, huku ukifungua milango ya ushirikiano, teknolojia na rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya mazingira.
Hatua hii inaunga mkono azma ya kukuza Uchumi wa Buluu endelevu kwa manufaa ya watu na asili katika Ukanda wa Bahari ya Hindi Magharibi.



