*Ahimiza huduma za kidijitali, usimamizi madhubuti na fursa kwa vijana

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka SACCOS barani Afrika kuimarisha ukusanyaji wa akiba na kuzielekeza katika uwekezaji wenye tija ili kukuza biashara, kuongeza uzalishaji na kutengeneza ajira.

Amesema hayo leo, (Alhamisi Oktoba 15, 2026,) katika kongamano la 26 la Vyama vya Ushirika wa Kifedha SACCOS barani Afrika, linaloendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwa Niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema Afrika inapaswa kujenga uwezo wa kubadilisha akiba za wananchi kuwa uwekezaji, uwekezaji kuwa biashara, na biashara kuwa ajira na ustawi wa jamii. 

Amesisitiza kuwa Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) vina wajibu unaovuka utoaji wa huduma za kifedha na kugusa maendeleo ya wananchi.

“Tusisubiri mustakabali wa maendeleo ujijenge wenyewe; ni lazima tuujenge mustakabali wetu. SACCOS zetu zinapaswa kuwa mstari wa mbele katika kubadilisha maisha ya wananchi, kuwawezesha vijana na kugeuza akiba kuwa uwekezaji wenye tija,” amesema.

Waziri Mkuu amehimiza matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kurahisisha huduma, kuongeza uwazi na kuwafikia wananchi wengi zaidi. Pia, amezitaka SACCOS kuwapa vijana fursa za kupata mikopo, ujuzi na kushiriki katika uongozi, akisema ushiriki wao ni muhimu katika kujenga uchumi wa baadaye.

Kuhusu usimamizi, amesisitiza uaminifu, uwajibikaji na weledi kwa viongozi na watendaji, pamoja na wanachama kurejesha mikopo kwa wakati. Amesema nidhamu ya kifedha na uwazi ni muhimu katika kulinda akiba za wanachama na kuhakikisha vyama hivyo vinakuwa imara na endelevu.

Ametaja mafanikio ya SACCOS katika kuwawezesha wakulima kugharamia uzalishaji, familia kusomesha watoto, wafanyakazi kujenga nyumba na wanawake na vijana kuanzisha biashara, kuwa ushahidi wa mchango wake katika ustawi wa jamii.

Akiongelea kaulimbiu ya mkutano huo, Waziri Mkuu amesema: “Kila kiongozi aliyepo hapa anao wajibu wa kufanya. Kwenye kila akaunti ya SACCOS kuna historia muhimu ya maisha ya mwanachama. Kwenye kila mkopo, kuna matarajio, Kwenye kila ushirika kuna jamii ambayo inatuamini tuwajengee maisha bora. Na kwa karne nyingi, vyama vya ushirika vimethibitisha kanuni kuu ya Kiafrika kwamba watu wakiunganisha nguvu zao pamoja, chochote ambacho kilionekana kigumu huwa kinawezekana.”

Awali, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema Tanzania ina jumla ya mawakala 231 wa huduma za fedha kupitia simu za mkononi wanaohusishwa na SACCOS, huku akisisitiza kuwa ubunifu unapaswa kwenda sambamba na maboresho ya teknolojia, usalama wa taarifa na ulinzi wa wateja.

Ameongeza kuwa, Tanzania ina SACCOS 981 zenye wanachama zaidi ya milioni 1.9 na mzunguko wa fedha unaozidi Sh. trilioni 1.6. Amehimiza ubunifu unaoendana na maboresho ya teknolojia, usalama wa taarifa na ulinzi wa wateja.