Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Rukwa
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema asilimia 90 ya wafanyakazi wanaotekeleza mradi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Malangali mkoani Rukwa ni Watanzania, hatua inayochangia kuongeza ushiriki wa wataalamu wa ndani katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya nishati nchini.
Mhe. Salome ameyasema hayo Oktoba 15, 2026, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.
Amesema mradi huo ni sehemu ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuhakikisha mikoa yote nchini inaunganishwa na Gridi ya Taifa na kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Aidha, Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa majaribio ya mitambo ya kituo hicho yanatarajiwa kuanza katikati ya Novemba 2026, hatua itakayokaribisha kukamilika kwa mradi huo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya nishati na uchumi wa Mkoa wa Rukwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange, amesema ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 85.17, huku kazi za kuwasha na kuingiza umeme zikipangwa kukamilika Novemba 2026.
Kituo hicho kinajengwa na kampuni ya TBEA kutoka China kwa gharama ya shilingi bilioni 161.9. Kitakuwa na uwezo wa kupokea umeme wa kilovolti 400 na kuushusha katika misongo ya kilovolti 220, 66 na 33, kikiwa na transfoma nne na njia nane za kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Rukwa.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuchochea uwekezaji na ujenzi wa viwanda, kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na madini, pamoja na kufungua fursa mpya za ajira na biashara ya umeme katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.











