Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kibaha
Kamati ya Maafa ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imekutana kwa ajili ya kujadili na kutathmini maandalizi ya kukabiliana na mvua za El-Nino.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Faraja Maliga amezitaka idara zote zilizopo kwenye Kamati hiyo kuendelea kuchukua hatua madhubuti za maandalizi ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.
Amesema, Watendaji wa Mitaa na Kata wametakiwa kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi, kwa mfumo wa mwananchi mmoja mmoja juu ya namna ya kujikinga na athari za mvua hizo, ikiwemo kutokaa kwenye maeneo korofi na mabondeni.
Maliga amewataka, kuendelea kusisitiza Wafanyabiashara wote katika Manispaa ya Kibaha wanatakiwa kuhakikisha wanafanya usafi katika maeneo yao ya biashara na kutofunga mitaro ya maji kwa taka.
Aidha, amesema kama kuna wananchi wanaenda tofauti na maelekezo basi Sheria Ndogo za Halmashauri ziweze kutumika na kuwachukulia hatua na kutoa adhabu kwa wananchi na wafanyabiashara watakaokaidi maelekezo ya usafi na uhifadhi wa mazingira.
Katika kikao hicho wameonesha baadhi ya Kata ambazo ziko katika hatarishi ya mvua hizo ambazo ni Kata ya Picha ya Ndege, Kongowe, Viziwaziwa, Mbwawa na Mailimoja .
Kamati imesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Halmashauri na wananchi ni muhimu ili Manispaa ya Kibaha iwe salama kipindi chote cha mvua hizo






