• Askofu Kilaini ataka hilo lifundishwe shuleni na vyuoni
• Sheikh Kichwabutwa awataka viongozi wa dini kuwafuata vijana vyuoni
• Mtaalamu wa saikolojia aeleza athari za malezi na mfumo dume
Na Kulwa Karedia, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wakati matukio ya mauaji ya kikatili yakiendelea kuripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini, viongozi wa dini wamesema umefika wakati wa kuanzishwa kwa somo la maadili kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu.
Mbali na somo hilo, viongozi hao wameshauri kuwapo kwa utaratibu wa viongozi wa dini kutembelea vyuo vya kati na vikuu ili kuwafundisha vijana maadili na kuwasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali, zikiwamo zinazohusu uhusiano wa kimapenzi.
Viongozi hao wametoa kauli hizo kwa nyakati tofauti walipotafutwa na JAMHURI kuzungumzia matukio ya mauaji yanayoendelea kuripotiwa katika mikoa ya Arusha, Mara, Dar es Salaam, Dodoma na maeneo mengine nchini.
Askofu Msaidizi Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini, amesema umefika wakati serikali iweke utaratibu wa kufundisha somo la maadili shuleni na vyuoni ili watoto na vijana watambue athari za matendo yao.
“Umefika wakati serikali ianzishe mitaala ya somo la maadili kwa ajili ya kuwasaidia vijana wetu. Ni muhimu mno kuwa na somo hili. Lazima tuwe na maadili ya msingi yasiyofungamana na dini fulani, bali yanayolihusu taifa.
“Kwa mfano, kuheshimu uhai wa mtu na kutomfanyia mwingine jambo baya ni mambo ya msingi, wala si ya dini pekee.
“Maadili haya yaanzie kwa walimu wenyewe waliopewa dhamana hiyo, kwa sababu wapo ambao hawana maadili. Sasa watawafundishaje watoto wetu? Ndiyo maana unaweza kukuta mwalimu anampiga mtoto vibaya hadi kumuumiza. Hiyo si adhabu ya kumrekebisha, bali ni hasira zake.
“Tukiwa na walimu wa namna hiyo, watoto watajifunza nini? Tukibadili fikra za walimu, ninakuhakikishia mambo yatabadilika,” amesema.
Kuhusu mauaji yanayotokea katika ndoa, Askofu Kilaini amesema baadhi ya wanandoa wanaingia katika mahusiano bila maandalizi ya kutosha wala kuzingatia misingi ya imani na malezi yao.
“Vijana au watu wengi wanakutana kwa siku chache na kukubaliana kuishi pamoja bila kufuata misingi na maadili ya Kanisa au familia zao. Jambo hili ni hatari mno.
KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA OKTOBA 20 -26, 2026



