NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Uimarishaji wa viwango vya ubora wa nafaka na mazao ya jamii ya kunde unatajwa kuwa hatua muhimu ya kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa, huku wadau kutoka nchi 70 duniani wakikutana nchini kujadili namna ya kuboresha viwango hivyo.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 45 wa Kamati ya Kimataifa ya Viwango inayoshughulikia mazao hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Robert Ngwasi, amesema Tanzania itatumia mkutano huo kubadilishana uzoefu na wadau wa kimataifa ili kuimarisha ubora wa mazao na kukuza biashara ya nchi.
Ngwasi amesema maandalizi ya viwango ni sehemu muhimu ya maendeleo ya sekta ya kilimo na biashara, kwa kuwa yanasaidia kuhakikisha mazao yanayozalishwa nchini yanakidhi mahitaji ya soko na kuwa na uwezo wa kushindana na bidhaa kutoka nchi nyingine.
“Tanzania imepiga hatua kubwa katika eneo la uandaaji wa viwango na kuwawezesha wakulima kuzalisha mazao yanayofaa na yanayoweza kuhimili ushindani katika soko huria,” amesema.
Ameeleza kuwa ubora wa mazao na bidhaa zinazozalishwa nchini umechangia kuijengea Tanzania heshima katika biashara, hivyo kuendelea kuimarisha viwango kutasaidia zaidi kuongeza ushindani wa bidhaa hizo katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Aidha, amesema Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo kwa mara ya kwanza barani Afrika, fursa inayoiwezesha nchi kushiriki katika majadiliano ya kimataifa kuhusu viwango, kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za kuimarisha ubora wa mazao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uandaaji Viwango wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Candida Shirima, amesema shirika hilo huzingatia mahitaji ya wadau katika ngazi mbalimbali wakati wa kuandaa viwango, yakiwemo ya kikanda, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), bara la Afrika na viwango vya kimataifa vinavyotolewa na Shirika la Kimataifa la Viwango (ISO).
Amesema TBS hushirikiana na wataalamu kutoka vituo vya utafiti, vyuo vya elimu ya juu, taasisi za utafiti na udhibiti, sekta binafsi pamoja na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi katika kuandaa viwango vinavyokidhi mahitaji ya masoko.
Aidha amesema ushirikiano huo unalenga kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakidhi matakwa ya viwango vya kimataifa na kuuzwa katika masoko mbalimbali bila vikwazo vinavyoweza kuzuiwa kupitia uboreshaji wa viwango.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kukuza biashara, kupanua fursa za masoko kwa wazalishaji wa ndani na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.







