WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amependekeza kuanzishwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Taasisi ya Tuzo ya Chakula Duniani (World Food Prize Foundation) ili kuwawezesha vijana kupata mafunzo, kufanya utafiti na kujiajiri kupitia kilimo cha kisasa.
Uongozi wa taasisi hiyo umepokea pendekezo hilo na kueleza utayari wa kuendeleza majadiliano kuhusu uwezekano wa kuanzisha programu ya vijana inayojulikana kama Youth Institute nchini Tanzania.
Dkt. Mwigulu ametoa pendekezo hilo jana (Jumatano, Oktoba 21, 2026) wakati akizungumza na viongozi wakuu wa taasisi hiyo, wakiwemo Rais Bi. Mashal Husain na Mtendaji Mkuu, Bw. Tom Vilsack, kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue), jijini Des Moines, Jimbo la Iowa, Marekani.
Waziri Mkuu alisema Tanzania inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo na taasisi zake za utafiti wa kilimo na washirika wa kimataifa ili vijana wa Kitanzania wanufaike na maarifa, teknolojia na uzoefu wa kuendesha kilimo kama biashara.
Alisema Serikali imeendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili vijana katika sekta ya kilimo, zikiwemo upatikanaji wa ardhi, mitaji na mikopo, pamoja na kubadili mtazamo wa kukiona kilimo kuwa shughuli ya watu waliokosa fursa nyingine.
Alieleza kuwa mafanikio ya baadhi ya vijana walioanzisha kampuni na kuajiri wenzao yamedhihirisha fursa zilizopo katika kilimo cha kisasa na uwezo wa sekta hiyo kuzalisha ajira na kuongeza kipato.
Kwa upande wake, Rais wa Taasisi ya Tuzo ya Chakula Duniani, Mashal Husain, alisema programu ya Youth Institute huwajengea wanafunzi uwezo wa kufanya utafiti na kupendekeza suluhisho la changamoto za chakula na kilimo, huku washiriki wanaofanya vizuri wakipata fursa ya kushiriki katika programu za kimataifa.
Aidha, Dkt. Mwigulu aliiomba taasisi hiyo iangalie uwezekano wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa kikanda wa DialogueNEXT ambapo Bi. Husain alisema taasisi hiyo iko tayari kuendeleza majadiliano kuhusu uwezekano wa kufanyika nchini.
Naye, Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Tom Vilsack, amependekeza programu za mafunzo na ushauri kwa vijana ziunganishwe na upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu pamoja na masoko ili kuwasaidia kuanzisha na kukuza biashara za kilimo.
Waziri Mkuu ameelekeza timu za watalaamu walioko kwenye ziara hiyo, kupitia ubalozi wa Tanzania nchini Marekani na wizara zinazohusika, ziendeleze mawasiliano na taasisi hiyo ili kuyafanyia kazi maeneo ya ushirikiano yaliyojadiliwa.
Waziri Mkuu ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, Balozi wa Tanzania Washington, Dkt. Elsie Kanza na watendaji wengine wa Serikali.










