Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Watumishi wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) wamepatiwa mafunzo kuhusu haki na wajibu wa mtumishi wa umma, yenye lengo la kuimarisha nidhamu, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mafunzo hayo yaliyotolewa na Robert Lwanji kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma, wakati wa shughuli ya Ukaguzi wa Uzingatiaji wa Sheria inayoendelea.Ambapo Mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa wa watumishi kuhusu sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia utumishi wa umma, pamoja na umuhimu wa kuzizingatia katika mazingira ya kazi.
Akielezea haki za watumishi, Lwanji alitaja kupata likizo, mafunzo ya kitaaluma, kupandishwa vyeo wanapokidhi vigezo vilivyowekwa, matibabu na mafao ya kustaafu kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi wa umma.
Alisisitiza kuwa haki hizo zinapaswa kuendana na utekelezaji wa wajibu, ikiwemo kuheshimu sheria na taratibu za kazi, kuwahi kazini, kufanya kazi kwa bidii na uadilifu, kutunza rasilimali za Serikali na taasisi, pamoja na kutoa huduma bora kwa wadau bila upendeleo.
Aidha, aliwahimiza watumishi kutunza siri za Serikali, kujiendeleza kitaaluma, kuheshimu viongozi na wafanyakazi wenzao, na kudumisha mahusiano mazuri kazini. Alionya kuwa ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma unaweza kusababisha hatua za kinidhamu kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwajengea watumishi wa PBPA uelewa mpana wa haki zao na wajibu wao, huku yakichangia kuimarisha nidhamu, uwajibikaji na utendaji wenye tija. Hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha Wakala unaendelea kutoa huduma bora kwa wadau na wananchi kwa kuzingatia misingi ya uadilifu, uwazi na weledi.








