Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri mvua za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mbalimbali nchini kuanzia Novemba mwaka huu hadi Aprili 2027, huku wananchi na taasisi mbalimbali zikitakiwa kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 23, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa na kusini mwa Morogoro inatarajiwa kupata mvua hizo. Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Amesema mwelekeo huo wa mvua katika maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka utaathiriwa kwa kiasi kikubwa na El Niño yenye nguvu kubwa, hasa kuanzia Novemba 2026 hadi Januari 2027. Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Oktoba katika baadhi ya maeneo ya Tabora, Katavi, Kigoma, Lindi na Mtwara, kabla ya kusambaa maeneo mengine mwezi Novemba na kumalizika kati ya wiki ya tatu na ya nne ya Aprili 2027.
Kwa mujibu wa Dkt. Chang’a, hali hiyo inachangiwa na ongezeko la joto la bahari katika eneo la tropiki ya kati ya Bahari ya Pasifiki, joto la bahari upande wa magharibi wa Bahari ya Hindi na upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo. Mifumo hiyo inatarajiwa kuongeza upatikanaji wa mvua, hivyo maandalizi ya mapema yanahitajika ili kupunguza athari zake.
Katika sekta ya kilimo, TMA imewashauri wakulima kuandaa mashamba mapema, kuchimba mifereji ya kupitisha maji na kutengeneza matuta ya kuzuia maji kutuama, huku wakitumia mbegu zinazofaa kwa mazingira ya maeneo yao. Kwa upande wa mifugo na uvuvi, mvua zinaweza kuongeza malisho, lakini wafugaji wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya milipuko, ikiwamo homa ya bonde la ufa.
Aidha, taasisi za usafirishaji na ujenzi zimetakiwa kukagua miundombinu mara kwa mara ili kupunguza uharibifu wa barabara, madaraja na reli za MGR na SGR. TMA pia imeeleza kuwa ongezeko la maji kwenye mabwawa linaweza kusaidia uzalishaji wa umeme, huku mamlaka za afya na maji zikitakiwa kulinda vyanzo vya maji na kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa ya milipuko.
Katika kukabiliana na majanga, menejimenti za maafa na serikali za mitaa zimetakiwa kuimarisha kamati za maafa kuanzia ngazi ya vijiji ili kuhakikisha tahadhari zinatolewa mapema. Wananchi wametakiwa kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 na mwezi unaotolewa na TMA, huku vyombo vya habari vikihimizwa kusambaza taarifa rasmi za mamlaka hiyo pekee.
TMA imekumbusha kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019, ni kosa kisheria kusambaza taarifa za hali ya hewa kutoka vyanzo visivyo rasmi, hivyo wananchi na wadau wote wanapaswa kutumia taarifa zinazotolewa na mamlaka hiyo kwa ajili ya kupanga shughuli zao na kuchukua tahadhari zinazofaa.










