Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Taasisi ya UKURASA Foundation inatarajia kuzindua mbio za Carry Your Tree , zinazojulikana kama “Beba Mti Wako”, Oktoba 31, mwaka huu,ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii kushiriki katika utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Taasisi hiyo imeiomba Serikali pamoja na wadau mbalimbali kujitokeza kuunga mkono mbio hizo ili kuimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira nchini kwa kuwarithisha vizazi vya sasa na vijavyo
Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika Salender Brige Club, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa UKURASA Foundation, Mhandisi wa mazingira Kiboko Manyerere, amesema mbio hizo zinatarajiwa kushirikisha zaidi ya watu 5,000, wakiwemo wananchi na watoto, kwa lengo la kujenga uelewa kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira.
Amesema mbio hizo zitafanyika Oktoba 31, zikianzia katika Viwanja vya Mnazi Mmoja na kuhitimishwa eneo la Daraja la Salender, ambako washiriki watashiriki zoezi la upandaji miti katika eneo la hifadhi ya mikoko.
Manyerere amesema mpango huo umeanzishwa kwa dhamira ya kuhamasisha jamii kuchukua hatua za vitendo katika uhifadhi wa mazingira, badala ya kuishia katika kutoa elimu pekee.
Amesisitiza kuwa kaulimbiu ya Carry Your Tree inalenga kuhimiza uwajibikaji wa pamoja katika kukabiliana na changamoto za kimazingira, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira.
Ameeleza kuwa washiriki watabeba miche ya miti wakati wa mbio hizo na kuifikisha katika eneo la Salender kwa ajili ya kupandwa, hatua inayolenga kuhamasisha wananchi kutambua umuhimu wa kupanda miti na kushiriki katika utunzaji wake.
Aidha, amesema wananchi wanaotaka kushiriki wanaweza kupata maelekezo kupitia kurasa za taasisi hiyo, huku ada ya ushiriki ikiwa Shilingi 10,000 kwa watu wazima na Shilingi 5,000 kwa watoto.
Kwa mujibu wa Manyerere, taasisi hiyo inatambua umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wananchi katika kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amewashukuru SAYONA,JIBUST , NATIONAL HOUSING, Taasisi ya Blue Carbon Tanzania wetoa miche hii ya mikoko na ndiyo wataalamu wa elimu ya uhifadhi wa mikoko
Pamoja na kuwashukuru TFS kukubali kutupa eneo la hifadhi ya msitu wa mikoko kwenda kupanda miche hiyo ya Mikoko kwenye eneo Salenda bridge na wadau na taasisi mbalimbali, zikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia Muungano na Mazingira pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kwa mchango wao katika kuwezesha maandalizi ya mbio hizo.
Amesema Kurasa Foundation inalenga kupanua wigo wa mbio hizo na kuzifikisha katika maeneo mengine, yakiwemo Zanzibar na Dodoma, ili kuhamasisha ushiriki mpana wa jamii katika uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam, Tulo Chilambo, amesema chama hicho kina wajibu wa kusimamia shughuli za riadha mkoani humo na kimepokea ombi la
UKURASA Foundation la kutumia mchezo huo kuhamasisha utunzaji wamazingira.
Chilambo amesema mbio hizo zitakuwa za kipekee kwa kuwa washiriki watakimbia au kutembea wakiwa wamebeba miche ya miti, ambayo itapandwa baada ya kufikishwa katika maeneo yaliyokusudiwa.
Ameeleza kuwa mbio hizo zitakuwa na makundi matatu, likiwemo la kilomita 10, litakaloanzia Mnazi Mmoja na kupitia eneo la Tanzanite Bridge kabla ya kuhitimishwa Salender, pamoja na kundi la kilomita tano litakalopita Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Aidha, amesema kutakuwa na mbio za kilomita mbili kwa watoto, zitakazofanyika katika eneo la Mnazi Mmoja, huku watoto wakipata nafasi ya kushiriki katika zoezi la upandaji miti.
Chilambo amewahimiza wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo, akisema zitatoa fursa ya kuunganisha michezo na juhudi za kulinda mazingira.
Pia ametoa wito kwa waandaaji kupanua shughuli hizo katika mikoa mingine ili kukuza vipaji vya vijana katika riadha na kuimarisha mwamko wa uhifadhi wa mazingira.
Amewapongeza wadhamini wa mbio hizo, akiwataja JIBUSTI ,SAYONA, National Housing na TFS kwa kuunga mkono mpango huo.

Naye Foibe Mchome, Mkuu wa Kitengo cha Mauzo kutoka SAYONA, amesema kampuni hiyo imeamua kudhamini mbio hizo kutokana na umuhimu wa upandaji miti na utunzaji wa mazingira katika jamii.
Mchome amesema upandaji miti unachangia kupunguza mmomonyoko wa udongo na kuboresha mazingira kwa ujumla, akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki. Ameongeza kuwa SAYONA itatoa vinywaji kwa washirikisiku ya tukio.
Kwa upande wake, meneja mauzo kutoka JIBUST Power Limited ErickLutazamba amesema kampuni hiyo itatoa huduma ya kukodisha vifaa vyakuhifadhi chaji za simu (power banks) kwa washiriki na wananchi watakaohitaji huduma hiyo, kwa gharama ya Shilingi 1,000.



