Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Manyara

SERIKALI imetoa maelekezo saba yanayolenga kupata ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro wa ardhi unaohusisha Wilaya za Chemba na Kiteto, ikiwemo kusitisha shughuli za kilimo ndani ya Hifadhi ya Wanyamapori Makame na kutenga ekari 1,200 katika Kijiji cha Ngamboro kwa ajili ya wakulima watakaostahili kupatiwa maeneo mbadala.

Maelekezo hayo yametolewa Oktoba 24, 2026, katika Kijiji cha Ndaleta, Wilaya ya Kiteto, Mkoa wa Manyara, na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, baada ya Serikali kukamilisha uchunguzi wa mgogoro huo na kuchambua maoni ya pande mbalimbali zilizohusika. Amesema maamuzi hayo yanalenga kuhakikisha ardhi inatumika kwa kuzingatia sheria, mipaka ya kiutawala na mipango ya matumizi ya ardhi.

 Dkt. Akwilapo amesema mpaka wa kiutawala kati ya Halmashauri za Wilaya za Chemba na Kiteto haujawahi kubadilishwa kama ilivyodaiwa, hivyo wananchi na viongozi wanapaswa kuutambua na kuuheshimu.

“Wananchi waliopewa maeneo ya kilimo ndani ya Hifadhi ya Wanyamapori Makame wanapaswa kusitisha shughuli zao, huku wale watakaostahili wakitambuliwa na kupangiwa maeneo mbadala katika ekari 1,200 zilizotengwa na Kijiji cha Ngamboro. “amesema Dkt. Akwilapo

Aidha, amesema maeneo yaliyotengwa katika mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji vya Makame, Irkisibor, Ndedo na Katikati yataendelea kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa, huku vijiji vinavyohusika vikielekezwa kuhuisha mipango yao ya matumizi ya ardhi na kuweka alama zinazoonekana wazi katika mipaka ya hifadhi ili kuzuia uvamizi na migogoro ya baadaye.

Waziri huyo pia amewataka viongozi wa vijiji kuhakikisha hawagawi ardhi nje ya mamlaka yao, akibainisha kuwa maeneo yanayodaiwa kugawiwa na vijiji vya Ndaleta na Mwitikia, maeneo ya Katikati na Ngamboro yalihusisha mamlaka ambazo hazikuwa na uwezo wa kisheria wa kuyagawa, hususan maeneo yaliyo nje ya mipaka ya vijiji au yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande, amewataka wananchi kupokea maamuzi ya Serikali kwa utulivu, kuheshimu maelekezo yaliyotolewa na kuendeleza ushirikiano ili kurejesha shughuli za maendeleo na kudumisha amani.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa maeneo husika katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Martin Shigela, amesisitiza umuhimu wa kusimamia matumizi sahihi ya ardhi na kuhakikisha ugawaji wa maeneo unazingatia mipaka na matumizi yaliyokubaliwa.

Amesema serikali itatoa maelekezo na mwongozo kwa halmashauri ili kuzuia kujirudia kwa makosa yanayohusiana na ugawaji wa ardhi, hususan maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za wananchi.

Shingela amewataka watendaji wa kata, wakuu wa wilaya, wakuu wa idara na viongozi wengine wa serikali kuhakikisha wanakomesha vitendo vya baadhi ya viongozi wa vijiji kutumia madaraka yao vibaya kwa kugawa maeneo ya malisho kwa ajili ya kilimo au maeneo ya kilimo kwa ajili ya malisho.

 Aidha ameonya kuwa watendaji wa serikali watakaokiuka maelekezo yaliyotolewa watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu zinazotumika.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa kuwatambua wananchi wanaopaswa kuhama kutoka maeneo yaliyopangwa kwa matumizi mengine na kuwahamishia katika eneo la hekta 1,200 lililotengwa kwa ajili yao.

Amesema zoezi hilo linapaswa kufanyika kwa kuzingatia misingi ya haki na usalama, bila upendeleo katika ugawaji wa ardhi. Ameeleza kuwa hakuna sababu ya mtu mmoja kupewa eneo kubwa huku wengine wakibaki na maeneo madogo yasiyolingana na mahitaji yao.

“Timu ya wataalamu ikiongozwa na Kamishna wa Ardhi itashirikiana na Mkuu wa Wilaya, kamati ya usalama na Mkurugenzi wa Halmashauri kutambua ukubwa wa eneo lililotengwa pamoja na kuandaa orodha ya wananchi wote wanaopaswa kuhamishwa. Amesema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha ardhi inagawiwa kwa usawa na wananchi wote wanaostahili wanapata maeneo yao kwa kuzingatia haki.”amesema Mhe.Shingela

Vilevile, amewataka wananchi kuwa wavumilivu na kutoa ushirikiano kwa serikali ili zoezi hilo likamilike kwa haraka kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua, hatua itakayowawezesha kupata maeneo ya kuzalisha.

Amesema wananchi wenye mahitaji mengine ya kiserikali wanapaswa kufuata njia rasmi kupitia kwa watendaji wa kata na vijiji, Mkuu wa Wilaya, madiwani, Mkurugenzi wa Halmashauri na mbunge ili kupata suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazowakabili.