Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, na Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, wametaka hatua za pamoja kuchukuliwa kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji, ikiwemo kutenga maeneo maalumu ya malisho, kusimamia matumizi ya ardhi na kuhakikisha kila kundi linafanya shughuli zake kwa kuzingatia sheria.
Nyongo ametoa maagizo mbalimbali katika mkoa huo, ikiwemo Chalinze, akiwataka wakuu wa wilaya kuhakikisha maeneo maalumu ya malisho ya mifugo yanatengwa ili kupunguza migogoro inayojirudia kati ya wakulima na wafugaji.
Amesema ameshatoa tamko la kutenga maeneo hayo, akisisitiza kuwa hataki kuona vitendo vya mauaji vinavyotokana na migogoro hiyo.
“Nimeshatoa tamko la kutenga maeneo hayo kuondoa magomvi hayo na katika mkoa wangu sitaki kuona mauaji ya wakulima na wafugaji, Nimeshamwambia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani sitaki kusikia mauaji, Tukifanya hivyo tutapunguza migogoro hiyo,” alisisitiza Nyongo.
Aidha, amewataka wakulima na wafugaji kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutumia kamati za usuluhishi kutatua changamoto zao kwa mujibu wa sheria.
Pia, amewaasa wakulima kuepuka kuwakaribisha wafugaji katika maeneo yao bila utaratibu unaokubalika, huku akiwataka wafugaji kuzingatia sheria na kanuni za ufugaji na kuepuka kuingiza mifugo katika mashamba ya watu na kuharibu mazao.
Kwa upande wake, Ridhiwani Kikwete aliwataka viongozi wa vijiji, Serikali na vyombo vinavyohusika kusimamia matumizi ya ardhi na kudhibiti uingizaji holela wa mifugo katika mashamba ya wakulima, akisisitiza umuhimu wa kulinda haki na shughuli za kiuchumi za kila kundi.
Kikwete alisema migogoro hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na ushindani wa matumizi ya ardhi, maji na malisho, pamoja na uhamaji wa wafugaji wanaotafuta rasilimali hizo.
Kutokana na hali hiyo, amependekeza kutengwa kwa maeneo maalumu ya kilimo na ufugaji, kusimamiwa kwa njia za mifugo na kusajiliwa kwa wakulima na wafugaji ili kurahisisha usimamizi wa shughuli zao.
Kadhalika anasisitiza umuhimu wa kuimarisha vikao vya ujirani mwema ili wakulima na wafugaji wapate fursa ya kujadili na kutatua changamoto zao kwa pamoja kabla hazijazua migogoro mikubwa.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, alisema Serikali imekuwa ikifanya operesheni za kukabiliana na migogoro ya ardhi, ikiwemo ile inayohusisha wakulima na wafugaji.
Anasema jitihada hizo zinaenda sambamba na kuhamasisha umoja, amani na kuheshimiana kwa kuzingatia maeneo na shughuli za kiuchumi za kila kundi.
Kwa upande wake, mfugaji wa Chalinze, Seleman Hassan, ameishukuru Serikali kwa kutoa elimu kwa wafugaji, akisema wataendelea kushirikiana na wakulima ili kuepuka kero zinazojitokeza baina yao na kuimarisha amani katika maeneo wanayoishi.
Migogoro ya wakulima na wafugaji imetajwa kuwa changamoto katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani, yakiwemo Chalinze, Bagamoyo, Rufiji, Kisarawe, Kibaha Vijijini na Kibiti







