NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimesisitiza umuhimu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti ya asili, huku kikijivunia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 65 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1961.

Akizungumza wakati wa zoezi la upandaji miti lililoandaliwa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 65 ya chuo hicho, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye, amesema chuo hicho kimepiga hatua kubwa katika kupanua huduma za elimu ya juu na kuchangia maendeleo ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Amesema chuo hicho kilichoanza mwaka 1961 kikiwa na wanafunzi 14, kimeendelea kukua na kupanua wigo wa shughuli zake katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Zanzibar, Dodoma, Nzega, Iringa na Mbeya, huku kikiendelea na mipango ya kufungua vituo Kagera na Lindi.

Amesema upanuzi huo ni ishara ya namna UDSM inavyogusa maisha ya Watanzania kupitia elimu ya juu, akisisitiza kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za waasisi wa taifa na viongozi mbalimbali waliokiunga mkono chuo hicho tangu kilipoanzishwa.

“Tunajivunia kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa letu. Wahitimu wa chuo hiki wamekuwa viongozi wakuu, mawaziri na watu mashuhuri ndani na nje ya Afrika. Hivyo, hatupaswi kujidharau, bali kuweka kifua mbele kwa kutambua mchango wetu,” amesema.

Ameongeza kuwa maadhimisho hayo ni fursa ya kutafakari safari ya chuo hicho, mafanikio yaliyopatikana na mwelekeo wake katika miaka 65 ijayo, huku zoezi la upandaji miti likiwa sehemu ya kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuweka kumbukumbu ya maadhimisho hayo.

Kwa upande wake, Prof. Samora Andrew kutoka idara ya elimu ya mimeo UDSM amesema upandaji miti ni muhimu kutokana na mchango wake katika kuboresha hewa, kutoa oksijeni na kusaidia kuhifadhi mazingira.

Amesema miti pia ni chanzo cha malighafi za ujenzi na nishati, hivyo jamii ina wajibu wa kuhakikisha inatunza mazingira kwa kupanda na kuhifadhi miti.

Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kupewa elimu kuhusu upandaji wa miti inayofaa kulingana na mazingira ya maeneo yao, akieleza kuwa katika ukanda wa pwani ni muhimu kuzingatia miti ya asili ambayo inaendana na mazingira husika.

Amehimiza jamii ya UDSM na Watanzania kwa ujumla kuifanya shughuli ya upandaji miti kuwa sehemu ya maisha ya kila siku badala ya kuitekeleza wakati wa maadhimisho pekee.