Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu, Mhandisi Imani Mruma, amesema Mkakati wa Taifa wa Matumizi Bora ya Nishati wa mwaka 2024–2034 umeweka malengo mbalimbali yanayolenga kuimarisha matumizi bora na yenye ufanisi ya nishati nchini.
Ameyasema hayo leo wakati akiwasilisha mada kuhusu mkakati huo katika Kongamano la Wiki ya Nishati Jadidifu linaloendelea katika Ukumbi wa EACLC, Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Akiwasilisha mada hiyo, ameelezea kuwa mkakati huo una malengo mbalimbali ikiwemo kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi bora na yenye ufanisi wa nishati pamoja na kuongeza ufanisi wa uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini kupitia utoaji wa elimu, usambazaji wa taarifa sahihi na uhamasishaji kuhusu teknolojia na mbinu bora za matumizi ya nishati.
Akifafanua jitihada za Serikali katika kutekeleza mkakati huo, Mhandisi Mruma ameeleza jitihada mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali pamoja na wadau, ikiwemo kuwajengea uwezo wanawake kuhusu matumizi bora ya nishati kupitia programu ya WISE (Women in Sustainable Energy), ambapo jumla ya wanawake 60 wa Kitanzania wamepatiwa ufadhili wa masomo ya Shahada ya Uzamili ya Uhandisi wa Nishati Endelevu kwa mwaka wa masomo 2023–2026.
Aidha, ameeleza juhudi zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kuhamasisha matumizi ya magari yanayotumia umeme (E-Mobility), ikiwa ni sehemu ya kuendeleza matumizi ya nishati safi ambazo ni rafiki kwa mazingira.







