Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dar es Salaam

SERIKALI imezitaka taasisi mbalimbali nchini kufanyia kazi mapungufu na changamoto zilizobainika katika zoezi la kitaifa la uigaji wa dharura za mafuriko yanayohusishwa na mvua za El Niño ili kuimarisha utayari na uwezo wa kukabiliana na maafa kabla hayajatokea.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Brigedia Jenerali Hosea Ndagala, wakati akifunga Zoezi la Kitaifa la Mezani la Uigaji wa Dharura kwa Taasisi Mbalimbali (SIMEX), lililofanyika kwa siku mbili Tanzania Bara.

Amesema zoezi hilo limekuwa muhimu katika kupima mipango ya utayari wa kukabiliana na dharura kuanzia ngazi ya taifa hadi ngazi za chini, hususan katika uratibu wa sekta mbalimbali, majukumu ya kitaasisi, usimamizi wa taarifa na uwezo wa kufanya maamuzi kwa wakati.

“Mapungufu na changamoto zilizobainishwa zisichukuliwe kuwa udhaifu, bali ziwe fursa muhimu za kuimarisha utayari wetu kabla maafa halisi hayajatokea,” amesema.

Amesema mafanikio ya zoezi hilo hayatapimwa kwa kukamilika kwa mafunzo hayo pekee, bali kwa namna taasisi zitakavyofanyia kazi mafunzo, uzoefu na mapendekezo yaliyopatikana ili kuboresha mifumo yao ya kukabiliana na dharura.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na washirika wa maendeleo pamoja na wadau wengine katika kuimarisha usimamizi wa vihatarishi vya maafa nchini.

Akihitimisha hotuba yake, Ndagala amesisitiza umuhimu wa kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza mapema, akitumia methali isemayo, “Usipoziba ufa, utajenga ukuta,” akieleza kuwa hatua za kurekebisha mapungufu zinapaswa kuchukuliwa kabla mvua halisi hazijanyesha.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jeshi la Polisi, ACP Deogratius Massawe, amesema jeshi hilo lina jukumu muhimu katika kongani ya utafutaji na uokoaji (Search and Rescue), ikiwemo kuhakikisha waathirika wa majanga wanakuwa salama wanapookolewa.

Amesema pamoja na jukumu hilo, Jeshi la Polisi lina wajibu wa kutoa ulinzi kwa waathirika, hususan watoto wanaoweza kutengana na wazazi au familia zao wakati wa majanga.

“Waweza kukuta familia zimetengana na watoto wametengana na wazazi wao. Kwa hiyo, jukumu la kuwalinda watoto kupitia Dawati la Jinsia la Polisi ni muhimu ili kuhakikisha hawafanyiwi vitendo vya ukatili au unyanyasaji, wanabaki salama na baadaye kuunganishwa na familia zao,” amesema.

Naye Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Kitengo cha Dharura na Maafa, Dkt.Simon Chacha, amesema mafunzo hayo ya mezani yaliyofanyika kwa siku mbili yamewezesha sekta mbalimbali na wadau kutathmini kiwango cha utayari wao katika kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Amesema kupitia zoezi hilo, washiriki wamepata fursa ya kutathmini maandalizi ya sekta mbalimbali, zikiwemo afya, ujenzi, miundombinu na kilimo, pamoja na kuangalia namna mipango iliyowekwa itakavyosaidia kukabiliana na dharura endapo mvua hizo zitatokea.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) nchini Tanzania, Bi. Christine Mendes,
amesema, Ofisi yake itaendelea kushirikiana na Serikali katika masuala ya usimamizi wa maafa nchini huku akikumbusha kila sekta kuwa na utayari katika eneo lake yanapotokea masuala la maafa.

“WFP itaendeleza ushirikiano katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini, pia nipongezee uwepo wa warsha hii ya siku mbili naamini itazaa matunda, itumike kwa vitendo kwa kujiandaa vyema kwani Maandalizi ni mazuri yanapunguza gharama za kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea,” alisema Bi. Christina