urlHoteli ya kitalii ya Ramada iliyopo Mbezi Beach, Dar es Salaam imeajiri wageni wasio na vibali vya kufanya kazi husika nchini.

Abdul Saleem Aboonhi Kollarathikkal, raia wa India mwenye hati ya kusafiria namba Z1873501 ameajiriwa katika Hoteli ya Ramada kama Mkurugenzi wa Fedha (Director of Finance), huku kibali chake kikionesha kitu kingine, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

Abdul alipatiwa kibali cha miaka miwili na Wizara ya Kazi namba WPQ/575/2015 kikibainisha kuwa ni Meneja Mfumo (System Manager) wa M/S. Beach Residence Ltd.

Kibali hicho kilichotolewa Januari 30, 2016 kitafikia ukomo Januari 29, 2018 na kimetiwa saini na Kamishna wa Kazi nchini.

Pamoja na mkurugenzi huyo, hoteli imeajiri raia kutoka nje ya nchi kwa kazi ambazo wazawa wanaweza kuzifanya na hazihitaji wataalamu kutoka nje ya nchi.

Baadhi ya kazi walizoomba kufanya lakini hawazifanyi na badala yake wanafanya kazi zilizoko kwenye mabano, ambazo zingeweza kufanywa na wazawa, ni kama ifuatavyo:

1.  Executive Housekeeper – Karuna Karan (usafi)

2.  Business Analyst-Front Office – Ramesh Sundar (yupo yupo tu)

3.  IT Support-Information and Telecommunication – Ramakrishnan P.N. (Duty Manager & Night Manager).

4.  System Economic Analyst – Sumed Prasanna (Msaidizi wa Mkurugenzi wa Fedha, kuandaa malipo ya mishahara).

5.  Revenue Analyst-Finance – Dhammika Siriwardana (kazi yake ni kujumlisha mauzo yote ya siku).

6.  Cost Analyst-Finance – Satish Bindu (Mtunza stoo).

7. Chef de Cuisine-Kitchen – Adham Adel (mpishi/mchoma nyama).

8. Wine Tester-F & B – Deeoak N (Muonja mvinyo).

9. African Restaurant Manager – Rajesh Mondar (Meneja Huduma ya vyakula na vinywaji – chakula cha Kiafrika).

JAMHURI haikupata ushirikiano kutoka kwa uongozi wa juu wa Ramada, kutokana na kutoruhusiwa kuonana na wahusika kwa maelezo kuwa wako nje ya ofisi kwa zaidi ya miezi miwili.

Hata hivyo, JAMHURI iliwasiliana na Afisa Rasilimali Watu aliyefahamika kwa jina moja la Mwanaidi, aliyesema yeye si msemaji wa hoteli hiyo na kwamba mwenye mamlaka ya kuzungumzia hilo ni bosi wake ambaye naye alikuwa nje ya ofisi.

Mwanaidi ameeleza kuwa yeye binafsi hahusiki na ajira za wageni hotelini hapo na kuwa hawezi kuzungumzia jambo hilo na iwapo JAMHURI inataka kupata ufafanuzi inapashwa kuiandikia hoteli hiyo maswali.

Afisa Uhusiano wa Ramada Hotel, Peter Kamanda, alipoulizwa kuhusiana na ajira hizo za wageni, aling’aka na kusema kuwa yeye ni mgeni hotelini hapo na hakuajiriwa kuzungumzia masuala ya wafanyakazi.

Amesema kazi yake ni “ushauri tu na hawezi kuzungumzia hilo”. Alipoulizwa nani hasa mwenye kutakiwa kulizungumzia amesema hajui na hawezi kujishughulisha na masuala hayo kwani hayamuhusu.

“Kwanza ninakushangaa kufuatilia mambo hayo usiyoelewa, mambo ya uongeaji wa ofisi siwezi kujua nani anapashwa kuongelea, tafuta ‘top management’ kwani unanipangia ya kusema? Sipo hapa kufanya kazi hiyo,” amesema Kamanda.

JAMHURI imewasiliana na Msemaji wa Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana, Ridhiwan Wema, kupata ufafanuzi kuhusiana na hatua zinazopashwa kuchukuliwa na wizara husika kwa wageni kufanya kazi ambazo zingeweza kufanywa na wazawa na matumizi ya kibali kwa kazi tofauti, akasema ni makosa na hairuhusiwi. Hata hivyo, amesema kwa sasa yuko likizo na mwenye mamlaka ya kuzungumzia jambo hilo kwa undani ni Afisa Kazi.

Afisa Kazi katika Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana, Omari Sama, alipoulizwa kuhusiana na kibali hicho amesema masuala ya vibali hayamuhusu. Kuhusiana na masuala kazi ambazo zingeweza kufanywa na wazawa kufanywa na wageni amesema kwa wakati huo alikuwa shamba na kwenye kikao hivyo asingeweza kuzungumza.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli, katika hotuba yake Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), alitoa agizo kwa raia wa kigeni walioajiriwa nchini kufuata sheria na akazitaka wizara zote kufichua wanaofanya kazi bila vibali na kulinda ajira za wazawa.

“Kushugulikia ajira za wageni wakati wazawa wapo, naagiza wizara zote zisimamie hili suala kwa nguvu zote, hata kwenye hoteli mtu anatoka nje, hili haliwezekani. Tumekuwa watu wa kushinikizwa na hawa watu,” alisema Rais Magufuli.

Hivi karibuni, Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana kupitia kwa Kamishna wake, Hilda Kabisa, kwa kushirikiana na baadhi ya maafisa, wamekuwa wakiendesha msako wa raia wa kigeni wanaofanya kazi nchini bila kufuata taratibu.

Hata hivyo, msako huo unaelezwa kukwamishwa na baadhi ya maafisa wa Uhamiaji waliogeuza wafanyakazi wa kigeni kuwa chanzo cha mapato wanaodaiwa kuchukua rushwa kwa wageni hao na kuacha mambo yakiendelea kama zamani.

By Jamhuri