Juni 25, mwaka huu, itakuwa imetimia miaka minane tangu Michael Jackson ‘Wacko Jacko’ alipoiaga dunia. Alikuwa ni mwanamuziki mwenye vipaji vingi kutoka nchini Marekani. Alifahamika zaidi kwa jina la heshima la ‘Mfalme wa Pop’.
Michael alitambulika kama mburudishaji aliyepata mafanikio zaidi kwa muda wote. Alikuwa mmoja kati ya waburudishaji wenye mvuto na hadhira kubwa katika medani ya muziki.
Michango yake katika muziki, fasheni, na hasa suala la kuanika hadharani maisha yake binafsi, vilimfanya awe kioo cha ulimwengu katika tamaduni maarufu kwa ziaidi ya miongo minne.
Wasifu wa Michael Jackson unaonesha kuwa alizaliwa Agosti 29, 1958 huko Gary, Indiana, nchini Marekani. Alitokea katika familia ya wanamuziki ya Jackson Five. Michael Jackson alifariki dunia Juni 25, 2009 katika hospitali ya UCLA Medical Center, nchini Marekani.
Wakati wa uhai wake, aliwahi kusimulia kuhusu miaka yake ya awali, mara kadhaa alisema kuwa baba yake alimlazimisha kufanya mazoezi mno ya kucheza na uimbaji.
Michael Jackson akiwa pamoja na ndugu zake, alishapewa uongozi wa uimbaji kwa mara ya kwanza akiwa kama mwanachama mdogo kabisa katika kundi la The Jackson 5, mwaka 1964. Alianza kazi ya usanii wa kujitegemea mwaka 1971.
Albamu yake ya mwaka 1982 iliyopewa jina la ‘Thriller’, imebaki kuwa  yenye mauzo bora kwa muda wote. Mchango wa Michael Jackson katika utengenezaji wa muziki wa video umeinua kutoka katika hali ya kawaida hadi katika hali ya kisanii zaidi.
Video zake za ‘Billie Jean, Beat It’ na ‘Thriller’ zilimfanya kuwa msanii Mmarekani Mweusi wa kwanza kupata kupigiwa nyimbo zake sana kwenye kituo cha televisheni cha MTV. Michael Jackson alipata umaarufu zaidi kwa baadhi ya mitindo yake ya kucheza muziki huo kama vile ‘Robot’ na ‘Moon Walk’.
Mitindo ya muziki, sauti yake na zile koregrafia, zimetambulika vizazi kwa vizazi hata katika mipaka ya kitamaduni. Alikuwa ni miongoni mwa wasanii wachache waliowekwa mara mbili kwenye ‘Rock and Roll Hall of Fame’.
Mafanikio mengine yamejumlisha tuzo ya ‘Guinness World Records’ (ikiwa ni pamoja Mburudishaji mwenye mafanikio kwa muda wote. Michael alituzwa tuzo za ‘Grammy 15’ – ikiwa ni pamoja na ile ya ‘Living Legend Award na ile ya Lifetime Achievement Award’.
Tuzo nyingine ni pamoja na ‘26 American Music Awards’ akiwa kama msanii pekee ya kujitegemea, pamoja na nyingine kwa ajili ya Msanii wa Karne, vibao vyake 17 vilishika nafasi ya kwanza huko nchini Marekani.
Msanii huyo anashikilia rekodi ya mauzo ya zaidi ya CD milioni 750 dunia nzima, inafanya kuwa miongoni mwa wasanii waliouza rekodi zao vilivyo kwa muda wote na haijawahi kutokea.
Katikati ya miaka ya 1980 muonekano wa Michael Jackson ulikuwa unabadilika bila kificho, umbo na sura yake vilibadilika pia, madaktari wa upasuaji kadhaa walikisia ya kwamba miaka ya 1990, alipitia upasuaji kadhaa wa pua, kuinua paji la uso, kufanya midomo iwe myembaba, na upasuaji wa mfupashavu.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa wasifu, J. Randy Taraborrelli, Jackson alifanya upasuaji wake wa pua kwa mara ya kwanza baada ya kuvunja pua yake wakati anacheza mchezo wa hatari mwaka 1979.
Hata hivyo, upasuaji huo haukukamilika vizuri, alianza kulalamika ya kwamba upumuaji wake ni wa tabu na utaathiri shughuli zake, akaelekezwa kwa Dk. Steven Hoefflin, ambaye alifanya upasuaji wake wa pua wa pili mwaka 1981.
Katherine Jackson, ingawa, alisema katika mahojiano yake ya kwamba Michael alipata madhila yake ya pua kwa makusudi hapo mara ya kwanza. Taraborrelli alieleza kwamba Michael Jackson alifanya tena upasuaji wa pua kwa mara ya tatu miaka mitatu baadaye na ya nne mwaka 1986.
Mwamba huyo wa Pop, Michael Jackson, aliandika katika wasifu wake mwaka 1988 ‘Moonwalk’ kwamba katika ongezeko la upasuaji wa pua, pia alipata kutengeneza kishimo (dimpo) katika kidevu chake.
Tangu mwaka 1986, Michael Jackson alikuwa mteja wa Arnold Klein, mtaalamu wa magonjwa ya ngozi ambaye amebobea katika tiba ya sindano za ugonjwa ngozi, utaratibu wa utoaji wa tiba ya upodozi bila upasuaji.
Katika kitabu chake, Michael, alidhani mabadiliko ya sura yake ni matokeo ya kubalehe, mpangalio mkali wa mlo wa kutokula nyama, upungufu wa uzito, badiliko katika mtindo wa nywele.

>>ITAENDELEA

By Jamhuri