Kila nikifikiria safari ilivyo, naona kama tupo mbali sana kufika mwisho, tupo njiani kwa safari ambayo hatima yake huenda tukafika salama na tukiwa na afya njema kabisa. Leo nimewaza mengi sana na nimekumbuka mengi sana; sina hakika kama mwishowe yatakuwa haya ninayowaza na ninayotaka niwashirikishe muyajue.
Nimewaza ile jeuri ya zamani ya kila mtu kuwa mkubwa katika dunia hii ya Tanzania, enzi zile za ‘unanijua mimi’? Enzi za ‘nitaongea na bosi wako’, ni kipindi ambacho kila mfanyakazi alikipitia kwa ugumu wake, wapo wafanyakazi ambao wanakumbuka madhila yale na athari kubwa ambazo ziliwakumba. Poleni mlioteseka na ninaona dalili za kufika safari tukiwa hatujuani isipokuwa ni mwendo wa  adabu na kuheshimiana tu.
Nimewaza jeuri ya pesa ya dili ambayo ilikuwa ikitutesa siye akina pangu pakavu, kauka nikuvae na wale waliokuwa wakijulikana kama mboga saba, hakika tumepitia katika maswahibu magumu sana ambayo ni vema tukawa na kumbukumbu kwa ajili ya vizazi vijavyo, ni kipindi ambacho wasio na dili waliona kama wanaishi kwa kudra za Mwenyezi Mungu.
Nimewaza jinsi nchi yetu ilivyokuwa shamba la bibi miaka michache iliyopita, na jinsi sasa wavunaji wanavyoangalia shamba kwa mbali, naona uzalendo wetu kama unatunyemelea kurudi huku baadhi wakitafuta namna ya kuwa waungwana katika uporaji na uvunaji shamba ambalo ni letu sote.
Mambo bado yanabana lakini kila mtu bado anawajibika katika nafasi aliyopo kuhakikisha kuwa safari yake atafika japo kuna mtikisiko mkubwa katika mabadiliko tunayokwenda nayo. Hakuna tena njia ya mkato na hakuna kubebana katika safari ya hapa kazi tu.
Nimewaza maisha ya baadhi ya wapiga dili kuwa na familia kubwa kutokana na kufuru ya fedha, sasa wapiga dili  wamezikimbia familia hizo na kuziacha zikiteseka kutokana na wao kubweteka kipindi cha dili na kuwa tegemezi kwa maana ya kula kulala, hawakujua kuwa kuna siku kutakuja kuwa na  safari ya kurudi kunako maisha halisi ya kufanya kazi.
Nawaza juu ya mabadiliko ya suala la usafiri, sheria na taratibu zake na utii wa sheria bila shuruti, ni mabadiliko makubwa sana. Ni miaka michache tu madereva walikuwa hawasikii la mwadhini wala la mnadi swala, sheria ilikuwa kwa ajili ya wengine na siyo wao, suala la mwendo mkali kwa miaka michache ilikuwa sifa ya dereva, abiria tulikuwa wahanga katika hili lakini leo ni historia kwa madereva wote kuanzia magari madogo hadi makubwa, sheria imeshika mkondo wake.
Nawaza juu ya suala la kodi lilivyokuwa likiendesha wakubwa wengi kulinasua, wapo ambao walidiriki kuachana nalo baada ya kuchoka au kutishwa na wenye nguvu ya pesa, wapo waliokuwa wana uwezo wa kuingiza mzigo wowote bila kulipia kodi na wapo waliokuwa wana uwezo wa kutoa bidhaa na kuziuza nje bila kuulizwa kodi. Hii ndiyo safari ninayoiona tukienda tukiwa na afua ya mafanikio ya kufika.
Nawaza jinsi nchi yetu ilivyokuwa ikimiliki midege mikubwa enzi hizo na umaskini wa ghafla wa kutokuwa na ndege nyingi, tulikuwa na kijidege kimoja kikiruka kutangaza jina tu lakini hakiwezi  kuliendesha shirika na jinsi sasa tulivyoanza kujikongoja na kuwa na ndege kadhaa zinazoweza kuendesha shirika, wapo wanaoponda lakini ukweli unabaki palepale kuwa safari imeanza na mafanikio yatapatikana.
Nawaona wenye matumaini mapya hata kama yatachelewa lakini tumeanza kuelekea kwa kasi nzuri, najua kuna upungufu mkubwa katika utekelezaji kwa kuwa baadhi wenye mawazo yale ya zamani tunao ndani ya safari, kazi kubwa ni kuhakikisha tunawaondoa katika chombo chetu ili tufike salama. Uongozi ni taasisi yenye mjumuisho wa watu wengi na fikra na ushauri wa wengi ili tufike salama. 
Safari ni ndefu lakini ina kila dalili ya mafanikio japo mambo ni mengi na vikwazo ni vingi, kuna mambo katika elimu, afya, ustawi wa jamii, miundombinu, nishati na madini, usafiri, teknolojia, maji, kilimo, uvuvi na sekta nyingine nyingi.

Wasaalam
Mzee Zuzu
Kipatimo.

By Jamhuri