- Aipa Tano Tume ya Madini ukusanyaji maduhuli
NAIBU Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amesema chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan Sekta ya Madini imepiga hatua kubwa.
Dkt. Kiruswa ameyasema hayo leo Aprili 30, 2025 wakati akifunga Kikao cha Manejimenti ya Tume ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma.
Amesema, kutokana na usimamizi mzuri wa Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, Naibu Katibu Mkuu, Msafiri Mbibo mafanikio makubwa yamepatikana katika Sekta ya Madini yaliyopelekea mchango wake kufikia asilimia 10.1 kwenye Pato la Taifa.

Katika hatua nyingine, amewapongeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwa kasi ya ukusanyaji wa maduhuli na kuwataka kuimarisha ushirikiano kati yao na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika Sekta ya Madini na kutatua kero za wadau wa madini.
“Nitumie nafasi hii kuwakumbusha umuhimu wa kushirikiana kutekeleza mikakati ya Usimamizi wa Sekta ya Madini ili sote kwa pamoja tuweze kufurahia ushindi wa kufikia malengo tuliyojiwekea,”amesema Dkt. Kiruswa na kuongeza,
*Nitoe rai kwenu kuongeza ushirikiano, mshikamano na upendo katika utendaji wa kazi ili tujenge nguzo imara itakayoendelea kutoa matokeo bora kwa Wizara yetu na kwa manufaa ya Taifa letu,” amesema.

Aidha, amewapongeza Menejimenti na Watumishi wa Tume kwa juhudi za ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo kuanzia kipindi cha mwezi Julai 2024 hadi Aprili 29, 2025 Tume imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 862.64 ikiwa ni asilimia 86.53 ya lengo la mwaka 2024/2025.







