Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Dalaam

Mamlaka ya Vitambulisho Vya Taifa (NIDA) ,imefanikiwa kumkamata mtu aliyekuwa anajihusisha na utengenezaji vitambulisho feki kwa Wananchi Danford Mathias mkazi wa Chalinze mkoani Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari msemaji wa mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA)Geofrey Tengeneza, amesema NIDA imefanikiwa kumkatama mtu ambaye amekuwa akijiihusisha na utengenezaji feki wa vitambulisho vya taifa kwa wananchi wenye namba za utambulisho NIN.

Tengeneza amedai kwa miezi kadhaa sasa kumekuwa na wimbi kubwa la watu walioibuka na kuwatapeli wananchi kwa kujinadi kuwa wanaweza kuwapatia wananchi huduma zitolewazo na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Amesema baada la wimbi hilo NIDA ilimua kuanza operesheni ambapo,tarehe 23/04/2025 saa 9.00 alasiri wakishirikiana na jeshi la Polisi walifanikiwa kumkamata Danford Mathias

“Mtu huyo aliyekuwa akijjhusisha na utengenezaji na uchapishaji wa Vitambulisho vya Taifa bandia,mpaka sasa bado anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi na hivi karibuniatafikishwa Mahakamani”Amesema.

Amedai wamefanikiwa kumkamata mtuhumiwa, baada ya kupata taarifa zake za kujihusisha na vitendo hivyo wakamwekea mtego ambao mwishowe walimnasa pamoja na vifaa vyake.

“Mtuhumiwa alikuwa akitengenezea wateja, vitambulisho feki katika steshenari yake iitwayo Bwanga studio iliyopo Msata Chalinze kwa malipo kati ya she 6,000/- па 10.000”Amesema.

“Katika mchakato wa utengenezaji vitambulisho hivyo feki , Mathias hutumia Kitambulisho chake halali cha NIDA na kuki-scan na kisha kukiingiza kwenye mfumo wa ADOBE na kufuta taarifa zake, na kubandika taarifa za mteja”Amedai.

Amesema imebainika kuwa katika Utengenezaji na uchapishaji wa Vitambulisho feki, baadhi ya watu wanaojishughulisha na biashara hii ni pamoja na wamiliki wa maduka ya steshenari.

Tengeneza ameongeza kuwa,wafanyabiashaa hao mbali na kijishughilisha na huduma ya steshenari kama ilivyo katika leseni zao , wamekuwa wakijihusisha na utengenezaji na uchapishaji vitambulisho vya Taifa feki kwa wananchi wenye Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN) kwa malipo ya fedha.

Amesema kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo, kwa sasa wameanzisha operesheni maalum ya kuwasaka na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wale wote wanaojihusisha na utapeli huo nchi nzima

“Napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha wamiliki wote wa maduka ya steshenari kutojihusisha kwa namna yeyote ile na utengenezaji au uchapishaji wa vitambulisho feki vya Taifa kwani kufanya hivyo, ni kosa la jinai”amesema.

Katika hatua nyingine NIDA, imefungia namba ambazo wahusika wametumiwa ujumbe wa wito wakuchukua vitambulisho vyao hawakwenda.

Tengeneza amesema namba inapofungwa, haina maana kwamba ndiyo basi utambulisho wako umefutwa, unatakiwa kwenda kuchukua Kitambulisho chako Namba yako inarudishwa (activated) na kuanza kutumika tena.

Amwesema operesheni hiyo itakuwa ni ya nchi nzima na endelevu kwani utapeli huo unafanyika sehemu mbalimbali