JESHI la Israel limeanza kuwaita makumi kwa maelfu ya askari wa akiba ili “kuimarisha na kupanua” operesheni zake huko Gaza.

Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema “linaongeza shinikizo” kwa lengo la kuwarejesha mateka waliokuwa wameshikiliwa huko Gaza na kuwashinda wanamgambo wa Hamas.

Wakosoaji wanasema mashambulizi ya hivi karibuni ya kijeshi, baada ya kusitishwa kwa usitishaji mapigano, yameshindwa kutoa hakikisho la kuachiliwa kwa mateka, na wanahoji malengo ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu katika mzozo huo.

Chini ya mpango huo, jeshi lilisema litafanya kazi katika maeneo mapya na “kuharibu miundombinu yote” juu na chini ya ardhi.

Vyombo vya habari vya Israel vinaripoti kuwa baraza la mawaziri la usalama la Israel limeidhinisha upanuzi mpya wa kijeshi huko Gaza.

Lakini ripoti zinaonesha kuwa halitafanyika hadi baada ya safari ya Rais Donald Trump katika eneo hilo wiki ijayo.

Mazungumzo ya kimataifa yameshindwa kufikia makubaliano mapya ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka 59 waliosalia wanaoshikiliwa na Hamas, 24 kati yao wanaaminika kuwa hai.

Hakuna mateka wa Israel aliyeachiliwa huru tangu Israel ianze tena mashambulizi yake tarehe 18 Machi.

Tangu wakati huo, Israel imeteka maeneo makubwa ya Gaza, na kuwafukuza tena mamia kwa maelfu ya watu wa Gaza.

Israel imesema lengo lake lilikuwa kuweka shinikizo kwa Hamas, mkakati ambao umejumuisha kuzuia misaada ya kibinadamu ambayo imekuwepo kwa zaidi ya miezi miwili.

Mashirika ya misaada, ambayo yameripoti uhaba mkubwa wa chakula, maji na dawa, yamesema hii ni sera ya njaa ambayo inaweza kuwa uhalifu wa kivita, madai ambayo Israel inayakataa.

Uvamizi uliopanuliwa utaweka shinikizo zaidi kwa askari wa akiba waliochoka, ambao baadhi yao wameandikishwa mara tano au sita tangu vita kuanza, na kufufua wasiwasi wa familia za mateka, ambao wameitaka serikali kufikia makubaliano na Hamas, wakisema hii ndiyo njia pekee ya kuokoa wale ambao bado wako hai.

Hatua hiyo pia itaibua maswali mapya kuhusu nia halisi ya Netanyahu huko Gaza.

Amekuwa akilaumiwa mara kwa mara na familia za mateka na wapinzani kwa kuhujumu mazungumzo ya makubaliano, na kurefusha vita kwa malengo ya kisiasa, tuhuma anazokanusha.