Rais wa Marekani Donald Trump ameamuru kufunguliwa tena na kutanuliwa kwa jela kubwa ya Alcatraz iliyokuwa ikitumika kuwafunga wahalifu waliotiwa hatiani kwa makosa ya kutisha.

Jela hiyo iliyokuwapo kwenye jimbo la California ilifungwa zaidi ya miaka 60 iliyopita na hivi sasa majengo yake yanatumika kama kivutio cha utalii.

Katika ujumbe kupitia mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema ameielekeza Idara ya Magereza nchini humo kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali kulifungua upya gereza hilo.

Amesema kwa muda mrefu, Marekani imezongwa na wimbi la “wahalifu watukutu wasio na mchango wowote kwa taifa zaidi ya kusababisha maafa na mateso kwa wengine.”

Trump amefafanua jela hiyo itawaondoa wahalifu wote ´wakaidi´ mitaani na kuwatenga kabisa na umma huku akiahidi Gereza la Alcatraz litakuwa “alama ya haki, utii wa sheria na mamlaka za dola.”