Na Deodatus Balile, JamhuriMedia,Dar es Salaam

Wiki iliyopita imekuwa na matukio makuu matatu. Mawili ni ya kusikitisha, na moja ni la faraja kwa watumishi wa umma wa taifa hili kuongezewa mshahara. Nalazimika kuyachanganya matukio haya, maana safu hii hutoka mara moja kwa wiki, nami sina utamaduni wa kuandika kwenye mitandao ya kijamii kabla ya siku ya safu. Nikiamini uzito wa andishi hili unapaswa kuendana na ratiba, mtanisamehe la mshahara nitaligusa kwa kifupi. Kuhusu mishahara, niseme tu ni jambo la heri kwa serikali kuongeza mishahara ya watumishi wake.

Sitanii, nijadili haya mawili; la kuumizwa kwa Padri Dk. Charles Kitima, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), na kutekwa kwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mdude Nyagali. Mambo haya yanaumiza mno. Yanaumiza si tu kutokana na maumivu waliyopata walioteswa au kutekwa, bali pia kwa sababu ya hatari kubwa ya kujenga nchi iliyojaa hofu.

Kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani Machi 19, 2021, nchi hii ilifika mahali ambapo ulipotoka nyumbani kwenda kazini hukuwa na uhakika wa kurejea nyumbani. Ulienea msamiati wa “watu wasiojulikana”. Matukio ya watu kutekwa na kuumizwa yalishamiri. Nakumbuka alivyotekwa na kuumizwa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka.

Dk. Charles Kitima, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Nakumbuka alivyotekwa na kurejeshwa katika mazingira ya kutatanisha mfanyabiashara mkubwa Mo Dewji. Nakumbuka alivyotekwa na kupotea milele mwandishi wa habari, Azory Gwanda. Nakumbuka alivyopotea bila maelezo kada wa CHADEMA, Ben Saanane. Sitagusia mauaji ya kinyama ya kina Alphonce Mawazo kule Geita.

Sitanii, nimeshangazwa na ujasiri wa kumvamia Padri Kitima katika makazi rasmi ya mapadri huko Kurasini, Dar es Salaam. Nimesikitishwa zaidi na taarifa ya polisi iliyotolewa na Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kutokana na maneno mawili yaliyochomekwa kwenye taarifa ya kuumizwa kwa Padri Kitima—kwamba alikuwa “anapata kinywaji.” Maneno haya yalilenga kumdhalilisha. Hayakubaliki.

Nikasikitika zaidi baada ya kuona kuna watu wanapata ujasiri wa kufoji nyaraka kuonyesha kuwa zimetolewa na Kanisa Katoliki, kumbe nazo ni feki. Kitendo cha kufoji waraka wa TEC kimethibitisha ni kwa kiwango gani maadili yamepungua katika jamii yetu. Pia, ujasiri wa kuingia makazi ya TEC, kumvamia na kumdhuru Padri Kitima, umethibitisha kiwango cha kushuka kwa hofu ya Mungu katika jamii yetu.

Jambo moja niliweke bayana, tunapaswa kupendana sisi Watanzania bila kujali itikadi za vyama vyetu, dini, kabila au jinsia. Napenda kumhakikishia kila mmoja kuwa sote ni marehemu watarajiwa. Kazi ya kuua tumwachie Mwenyezi Mungu anayefanya mavuno shambani mwake. Hata kama umetumwa ukamuue fulani au ukamuumize, ujue fika ipo siku nawe utakufa. Hakuna atakayeishi milele. Sasa kujipa jukumu la kuua au kuumiza mtu ni ishara kuwa mhusika hajitambui.

Mdude nadhani hii ni mara ya pili. Ukiacha kesi zake za hapa na pale, mwezi Mei mwaka 2019 alitangazwa kutekwa. Mdude alipatikana baada ya siku tatu. Inaarifiwa kuwa wanakijiji walimpata ametupwa katika kijiji cha Makwenje, Kata ya Inyala katika Jimbo la Mbeya. Kwa muda mrefu amekuwa na misukosuko.

Matukio ya watu kutekwa, kupotea kama kuku, kuumizwa na kuuawa tumekuwa tukiyasikia kwa majirani zetu kama Rwanda, Burundi, DRC na Kenya. Sisi hapa kwetu tumekuwa tukionekana kama kisiwa cha amani. Huyu mdudu aliyetuingia vichwani tangu mwaka 2016, tukaanza kuamini kuwa anayepingana na wewe njia pekee ni kumteka, kumuumiza au kumuua, tunapaswa kulipunga pepo hili liondoke.

Si heshima kwa taifa letu kugubikwa na matukio haya. Naamini serikali isipoyadhibiti, yataibua makundi ambayo yataisumbua nchi kama ilivyo kwa DRC ya sasa. Tukiwachekea wanaoyatenda, hata kama ni watu binafsi kwa masilahi binafsi, madhara yake mbele ya safari ni makubwa mno. Tuyakatae. Polisi nao wana wajibu wa kuyachunguza mambo haya na kuyatolea majibu hadharani haraka.

Sitanii, ni kweli matukio kama haya yanatokea katika nchi nyingi duniani ikiwemo hata Marekani, lakini tofauti yetu na Marekani ni mchakato wa uchunguzi. Hadi leo hatufahamu nani alimteka Dk. Ulimboka, nani alimmwagia tindikali Saed Kubenea, nani alimg’oa jicho Absalom Kibanda, nani alimuua Ali Kibao, nani alimteka Azory Gwanda. Wala hakuna aliyefikishwa mahakamani.

Kwa Marekani, jaribio la kumuua Donald Trump wakati wa kampeni nje ya uwanja wa golf, mhusika alifahamika ndani ya saa tatu na akafikishwa mahakamani. Najiuliza: tatizo hapa kwetu liko wapi? Hivi ni kweli polisi wetu hawana uwezo wa kufanya uchunguzi na kuwatia mbaroni wahalifu kwa wakati ili jamii iamini kuwa kodi zetu zinawalipa watumishi hawa kwa usahihi?

Narukia, tumeambiwa Dk. Kitima anaendelea vizuri. Waliomuumiza tunataka wasakwe na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Mdude naye asipotee kama kuku. Watanzania pia tujenge utamaduni wa kutoa taarifa. Siamini kama hakuna mtu anayefahamu kinachoendelea katika matukio haya mawili. Tuwe kama Wamarekani. Wana kaulimbiu: See Something, Say Something (Ona kitu, sema kitu).

Sitanii, tukiyaona mambo haya kisha tukayanyamazia, tunaweza kudhani ni ya Dk. Kitima na Mdude pekee, lakini ipo siku yatakuwa kwako na familia yako. Watanzania tusimame pamoja. Tukemee matukio ya aina hii. Iwe yanatokana na siasa au lolote liwalo, Watanzania tuna haki ya kuishi kwa amani. Kifo chetu kitokane na mapenzi ya Mungu na si vinginevyo. Watanzania tusimame pamoja kusema hapana; tunayakataa matukio haya. Polisi sakeni wahalifu hawa.
Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827