Waziri Mkuu wa Romania Marcel Ciolacu amejiuzulu jana jioni, siku moja baada ya mwanasiasa wa upinzani wa mrengo mkali wa kulia kushinda duru ya kwanza ya uchaguzi wa marudio wa rais.

Ciolacu alisema chama chake cha Social Democrats kinajiondoa kutoka muungano uliounda serikali yake, lakini mawaziri wanabakia kwenye nafasi zao hadi baada ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais itakapofanyika Mei 18.

Kwenye duru ya kwanza iliyofanyika Jumapili, mgombea wa chama Waziri Mkuu Ciolacu alishindwa na mwanasiasa wa mhafidhina George Simion aliyejipatia asilima 41 ya kura. Simion atachuana kwenye duru ya pili na mgombea aliyeshika nafasi ya pili ambaye pia ni Meya wa mji mkuu, Bucharest, Nicusor Dan.

Kujiuzulu kwa Ciolacu kunaweza kufungua njia ya kuundwa serikali mpya ya mrengo wa kulia yenye sera zinazoupinga Umoja wa Ulaya, ambao Romania ni mwanachama.