Moshi mweusi umetoka kwenye chimni ya Kanisa la Sistine ishara kuwa makadinali wameshindwa kumchagua kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki katika duru yao ya kwanza ya kura ya kongamano lao.
Makumi ya maelfu ya watu walikusanyika katika viwanja vya Mtakatifu Petro kusubiri kuona moshi huo, ambao ulitoka karibu saa tatu na dakika 15 baada ya makadinali 133 kujifungia kwenye mkutano wa faragha.
Makadinali hao waliondoka na kurudi kwenye makazi ya Santa Marta ambako wanakaa kwa ajili ya uchaguzi huo. Wataanza tena shughuli ya upigaji kura asubuhi hii.
Makadinali waliitwa Rome kufuata kifo cha Papa Francis mnamo Aprili 21 baada ya miaka 12 ya kuwaongoza Wakatoliki bilioni 1.4 ulimwenguni. Chini ya utamaduni huo wa karne nyingi, walio chini ya miaka 80 hupiga kura ya siri katika Kanisa la Sistine hadi mmoja wao atakapopata wingi wa theluthi mbili – kura 89 – ili kuchaguliwa kuwa papa.
Huku wakiwa wamejifungia ili kuepusha uingiliaji, mbinu yao pekee ya kutangaza matokeo yao ni kuchoma kura zao kwa kutumia kemikali maalum zinazotoa moshi.
Moshi mweusi unaashiria uamuzi haujafanyika, na kama ni mweupe ina maana papa mpya amepatikana. Kongamano hili la makadinali ndio kubwa kabisa na lenye sura ya kimataifa kabisa, likiwaleta Pamoja makardinali kutoka karibu nchi 70. Wengi wao hawakujuana kabla.
Hakuna anayepigiwa upatu kumrithi Muargentina mwenye haiba Papa Francis. Changamoto zinazoikabili taasisi hiyo iliyoanzishwa miaka 2,000 iliyopita ziko wazi.
Papa mpya atalazimika kukabiliana na hali ya kuweka usawa wa kidiplomasia katika wakati ambao kuna sintofahamu ya siasa za kikanda, pamoja na mgawanyiko mkubwa ndani ya Kanisa.

