Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Simiyu
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Simiyu Mei 7, 2025 ilimtia hatiani Mwalimu Emmanuel Pamba Evarist katika shauri la Uhujumu Uchumi namba 9350/2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Martha Mahumbuga, akiwepo Mwendesha Mashtaka Bi. Albertina Mwigilwa.
Shauri hili lilihusisha washtakiwa wawili ambao ni Emmanuel Pamba Evarist na MMANUEL PAMBA EVARIST na Bw. Zephania William Nhandala lakini mshtakiwa wa pili aliachiwa huru.
Mshtakiwa wa kwanza alikuwa anakabiliwa na mashtaka 6 ambayo ni Kuisababishia Mamlaka Hasara, kinyume na Aya ya 10(1) ya Jedwali la kwanza na vifungu 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, [Sura 200 R. E. 2022]; Kujipatia Fedha kwa Njia za Udanganyifu, Kughushi Nyaraka pamoja na Kuwasilisha Nyaraka za Uongo kinyume na Kanuni ya Adhabu [Sura 16 R. E. 2022]
Mshtakiwa wa kwanza akiwa ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Kilulu iliyopo Wilaya ya Bariadi Mkoani SIMIYU, alighushi nyaraka mbalimbali za utumishi kuonesha kuwa alikuwa na umri wa miaka 55 hivyo kuziwasilisha ofisi ya PSSSF (M) Simiyu ili aweze kulipwa mafao wakati hakuwa na umri huo na hivyo hakustahili kulipwa mafao yoyote kwa wakati huo.
Mshtakiwa kwa njia za udanganyifu alilipwa fedha hizo kama mafao kinyume na Sheria.
Lakini pamoja na kulipwa fedha hizo huku PSSSF wakiamini ni mafao stahiki, mshtakiwa aliendelea na kazi huku akiendelea kulipwa mishahara kila mwezi pamoja na fedha ya kila mwezi ya kiinua mgongo.
Akiendesha shauri hili Mwendesha Mashtaka Bw. Bahati Madoshi Kulwa alifanikisha upande wa Jamhuri kuthibitisha mashtaka yote sita (6) yaliyokuwa yanamkabili mshtakiwa huyo.
Mshtakiwa alihukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa kosa la kwanza la kuisababishia Mamlaka hasara, miaka 7 jela kwa kila kosa kwa makosa mengine yote matano. Adhabu zote zinakwenda sambamba.
Vile vile, Mahakama iliamuamuru mshtakiwa kulipa haraka iwezekanavyo fedha zote jumla ya TSH. 70,317,644.44 alizoisababishia Mamlaka hasara.
