Ukraine imesema iko tayari kwa usitishaji mapigano na Urusi kwa muda wa siku 30 kuanzia siku ya Jumatatu.
Hayo yameelezwa na waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo Andrii Sybiha katika wakati viongozi wa mataifa manne ya Ulaya wako mjini Kyiv kwa ziara ya kuonesha mshikamano na taifa hilo lililo vitani.
“Ukraine na washirika wake wako tayari kusimamisha mapigano bila masharti yoyote, kwa maana ya ardhini, angani na baharini kwa muda wa siku 30 kuanzia Jumatatu”, ameandika waziri Sybiha kupitia mtandao wa kijamii wa X.
“Iwapo Urusi itakubali na usimamizi kamili wa makubaliano hayo utahakikishwa, usitishaji mapigano na njia za kuimarisha imani ya kila upande, vitafungua njia ya kuanza mashauriano ya uhakika ya amani,” ameongeza mwanadipomasia hiyo.
