Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha
Wadau kutoka sekta ya bima nchini na nje ya nchi wameungana pamoja kutafakari changamoto na mambo mbalimbali ya kisekta ili kuanzisha msingi thabiti wa kuondokana na changamoto za udanganyifu katika soko la bima.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Umoja wa Wataalam wa masuala ya uchunguzi na ubadhirifu wa masuala ya Bima (IASIU), Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt Sada Mkuya amesema mkutano huo umekuja na suluhisho la masuala ya udanganyifu na kufanya soko kuwa endelevu na wateja wa bima kupata stahiki zao bila udanganyifu wowote lakini pia kampuni za bima zitakuwa na mazingira rafiki ya kufanya biashara na uwekezaji.

Akimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Dkt. Mkuya amesema takribani asilimia 10 hadi 15 ya madai ya bima duniani kote yana viashiria vya udanganyifu hali inayosababisha changamoto kubwa kwa kampuni za bima pamoja na serikali.
“Mkutano huu utajadili kwa kina tatizo sugu la udanganyifu linaloendelea na kukuwa katika sekta ya bima, udanganyifu huu umeathiri kwa kiasi kikubwa uaminifu wa sekta hii na kunaongeza gharama za huduma kwa kampuni za bima, unadhoofisha uwekezaji, na unaathiri ustawi wa wananchi wetu ambao wanategemea bima kama ngao ya kiuchumi dhidi ya majanga” amesema Dkt. Mkuya.
Amesema udanganyifu wa bima si tu ni kosa la jinai bali pia ni kosa la uhujumu uchumi ambalo ni kikwazo cha maendeleo kinachoporomosha imani ya wananchi katika mfumo, unaongeza gharama za huduma kwa wateja wa kweli na unaathiri uendelevu wa kampuni za bima ambazo zinafanya kazi kwa uadilifu.
Amesema nchi yaTanzania imeshuhudia ongezeko la visa vya madai hewa, matumizi ya nyaraka bandia, uwasilishaji wa madai ya uongo au ya kupangwa, kuficha taarifa muhimu wakati wa kuomba bima,
ushirikiano usio sahihi kati ya wateja na watumishi wa kampuni za bima.

“Hili haliwezi kuvumiliwa kwa sababu fedha hizi hupotea ambazo zingetumika kutoa huduma bora kwa wananchi au kuongeza uwekezaji katika maeneo mengine ya maendeleo hivyo ni muhimu kuweka kanuni kali dhidi ya kampuni au watu binafsi wanaojihusisha na udanganyifu pamoja na kuanzisha mahakama au kitengo maalum cha kushughulikia kesi za udanganyifu wa bima kwa haraka na kwa weledi”
Kamishna wa Bima nchini Dkt. Baghayo Saqware amesema udanganyifu kwenye sekta hiyo unaendelea kuwa mwiba na kwamba watashirikiana kwa njia zote kuhakikisha tunaondoka aina zote za udanganyifu na ubadhirifu kwenye bima.
Amesema wameunda kitengo cha kuchunguza udanganyifu na ubadhirifu pamoja na kuweka mikakati na miongozo thabiti ili kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi kwa weledi ili wananchi wapate huduma inayostahili.
“Mbali na hayo lakini tunaendelea kutoa elimu ya Bima ili kukabiliana na wahalifu ingawa nao wanabuni mbinu mbalimbali za udanganyifu kila siku, tutajifunza kutoka Kwa wenzetu njia bora ya kupambana nao” amesema Dkt. Saqware.
Aidha amesema bima itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ikiwemo kuandaa kanuni na miongozo ya kusimamia soko la bima, kulinda haki za wateja wa bima pamoja na kutoa elimu ya Bima Kwa Umma.

Rais wa IASUI tawi la Tanzania Mjabwa Hanzuruni ameomba ushirikiano kutoka sekta za Umma na binafsi ili kujenga misingi ya uwazi na uaminifu kwa Taasisi hizo.
Amesema IASIU inalenga kuweka msisitizo mkubwa juu ya umuhimu wa kuwepo kwa vitengo imara vya uchunguzi ndani ya taasisi za kifedha na bima pamoja na kuweka mifumo ya kuripoti na kushughulikia madai yenye mashaka.