Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amegomea mazumgumzo ya amani yaliopangwa nchini Uturuki baada ya Rais wa Urusi Vladmir Putin kutojitokeza na badala yake viongozi hao wamewakilishwa na maafisa wa chini.

Ametangaza kuwa hatashiriki mazungumzo ya amani yanayotarajiwa kufanyika leo mjini Istanbul, Uturuki, kati ya Ukraine na Urusi. Badala yake, ujumbe wa Kyiv utaongozwa na Waziri wa Ulinzi Rustem Umerov.

Uamuzi huo wa Zelensky umejiri baada ya Urusi kuthibitisha kuwa Rais Vladimir Putin hatohudhuria kikao hicho, na badala yake ametuma kile ambacho Zelensky ameita “maafisa wa ngazi ya chini.”

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Ankara baada ya kukutana na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, Zelensky alisema hana sababu ya kusafiri hadi Istanbul ikiwa Putin mwenyewe hatakuwepo.

“Tutasubiri taarifa kutoka Marekani na Uturuki kuhusu muda kamili wa kikao,” alisema Zelensky. “Urusi haionekani kujali sana kuhusu mazungumzo haya. Lakini bado niko tayari kwa mazungumzo ya ana kwa ana na Rais Putin”

Pamoja na hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, amesema kuna dalili za matumaini kufanyika kwa mazungumzo ya ana kwa ana, ingawa misimamo ya pande mbili bado inatofautiana.

Pande zote mbili kimsingi zimeonyesha kukubali wazo la kusitisha mapigano,” alisema Fidan. “Hata hivyo, wana mitazamo tofauti kuhusu jinsi ya kutekeleza hatua hiyo. Ukraine inataka usitishaji vita wa haraka na usio na masharti, lakini Urusi inasisitiza kuwa baadhi ya masuala lazima yakamilishwe kwanza.”