Na Mwandishi Wetu, JamahuriMedia, Morogoro
Rais wa Zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki ametembelea eneo la kihistoria la Mazimbu, lililoko mkoani Morogoro ikiwa ni katika Maadhimisho ya Siku ya Afrika ambayo huadhimishwa Mei 25 kila mwaka.
Ziara hiyo maalum imebeba uzito mkubwa wa kihistoria na kiishara, ikikumbusha mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi kwa Afrika Kusini wakati wa mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo.
Eneo la Mazimbu, ambalo sasa ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), lilikuwa makazi na kituo cha mafunzo kwa wapigania uhuru wa Chama cha African National Congress (ANC) kilichokuwa kinaongozwa na Hayati Nelson Mandela.

Katika ziara hiyo, Mbeki ametembelea makaburi ya wapigania uhuru waliofariki na kuzikwa katika eneo hilo na kuweka shada la maua, kupanda mti wa kumbukumbu na kutembelea hospitali ya SUA ambayo ilikuwa ikiwahudumia wapigania uhuru hao katika eneo la Mazimbu na kuzungumza na uongozi wa SUA ulioongozwa na Mkuu wa Chuo hicho, Mzee Joseph Warioba.
Mbeki ameahidi kuwa Taasisi yake kwa kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere itaandaa makala maalum ya picha mwendo kwa lengo la kuhifadhi na kuipeleka historia ya eneo hilo kwa wananchi wa Afrika Kusini ili wajionre mchango wa Tanzania kwao.
Akizungumza baada ya kuzuru makaburi hayo Mbeki ametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Tanzania na wananchi wake kwa uungwaji mkono usioyumba ambao walioutoa kwa ndugu zao wa Afrika Kusini wakati wa nyakati za dhiki.
“Mazimbu ni nyumbani kwetu, eneo hili si sehemu ya historia ya Afrika Kusini tu, bali ni alama ya mshikamano wa kweli wa Afrika. Tanzania ilisimama nasi wakati wa giza kuu la ukandamizaji. Leo tuko huru kwa sababu mlitupokea, mkatufundisha, na mkatupa hifadhi,” amesema Mbeki kwa hisia.

Taasisi ya Thabo Mbeki kwa kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere zimeandaa Maadhimisho ya Siku ya Afrika 2025 ambapo Mhadhara wa 15 wa Taasisi ya Thabo Mbeki utafanyika jijini Dar es Salaam Mei 24 kuadhimisha siku ya Afrika Kusini nchini.
Ziara hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Afrika, yanayoadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Mei, ikiwa ni kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika (zamani OAU) na kuhamasisha mshikamano, maendeleo na utambulisho wa bara la Afrika.
Mbeki yuko nchini pamoja na Taasisi ya Thabo Mbeki ambao wanashirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na Chuo Kikuu cha Afrika Kusini kuadhimisha ya Siku ya Afrika mwaka 2025.
Mei 25, 2025 Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Umoja wa Mabalozi wa Afrika (ADG) wamaeandaa mbio maalum zijulikanazo kama Afrika Day Marathon kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Afrika.
Mbio hizo za Kilomita 5, 10 na 21 zitaanzia katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam na kumalizikia hapo hapo.
