Na Mwandisi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa umeendelea kuimarika na kukua kutoka asilimia 7.3 mwaka 2021, asilimia 9.1 mwaka 2023 na kufikia asilimia 10.1 mwaka 2024.

Hayo yamebainishwa na leo Mei 24, 2025 na Waziri wa Madini,Athony Mavunde wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati akielezea mafanikio ya Serikali kwa kipindi cha miaka minne.

Amesema uwa sekta ya Madini imefanikiwa kuvuka lengo la kuchangia asilimia 10 kwenye Pato la Taifa mwaka mmoja kabla ya muda ulioainishwa katika Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/2022 hadi 2025/2026 na kufikia mchango wa asilimia 10.1 mwaka 2024.

Aidha, kasi ya ukuaji wa Sekta ya Madini umeongezeka kutoka asilimia 9.4 Mwaka 2021, asilimia 10.8 mwaka 2022 na kufikia asilimia 11.3 Mwaka 2023.

“Kama mnavyofahamu, moja ya majukumu ya Wizara ni kukusanya maduhuli ya Serikali. Katika kipindi husika, Serikali imeendelea kuboresha Sheria, kanuni na miundombinu mbalimbali ikiwemo umeme migodini hali ambayo imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuongeza ufanisi wa kazi katika shughuli za madini” amesema Waziri Mavunde.

Amesema uwa kutokana na hali hiyo, katika kipindi cha miaka minne ya Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan, maduhuli ya Serikali yamepanda kutoka Shilingi bilioni 623.24 Mwaka 2021/2022 hadi kufikia Shilingi bilioni 753.18 Mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 20.8 ya makusanyo kwa miaka mitatu.

Amesema kuwa aidha, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 Wizara ilipewa lengo la kukusanya Shilingi Trilioni Moja. Hadi kufikia tarehe 14 Mei 2025, Wizara ya Madini imefanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 902.78 sawa na asilimia 90.28 ya lengo la mwaka 2024/2025.

Mbali ya sekta hii kuchangia mapato ya yatokanayo ni maduhuli ya Serikali, Mchango wa Sekta ya Madini katika fedha za kigeni kwa mauzo yote ya bidhaa nje ya nchi umeendelea kuimarika kutoka Dola za Marekani bilioni 3.1 sawa na asilimia 45.9 mwaka 2021 hadi Dola za Marekani bilioni 3.55 sawa na asilimia 46.1 mwaka 2023.

Amesema kuwa upande wa mauzo ya bidhaa zisizo asilia (non-traditional goods), mchango wa sekta ya madini umeongezeka kutoka asilimia 53.8 mwaka 2021 hadi asilimia 56.2 mwaka 2023.

Amesema kuwa sekta hii ya madini imeajiri Watanzania wengi ikijumuisha ajira za moja kwa moja, wakandarasi na watoa huduma migodini. Wizara imeendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kuzalisha ajira zaidi kwa Watanzania kutoka kwenye kampuni mbalimbali za uchimbaji madini ambapo katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2023 Kampuni za uchimbaji madini ziliweza kuzalisha ajira 19,356 na kati ya hizo ajira 18,853 sawa na asilimia 97.40 ni Watanzania.

Vilevile, katika kipindi hicho jumla ya bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.9 ziliuzwa na kusambazwa migodini ambapo kati ya hizo Kampuni za Watanzania zilifanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.5 sawa na asilimia 92 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote na huduma zilizotolewa migodini.