Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waziri wa Madini, Athony Mavunde amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini mwaka 2019, Masoko na Vituo vya Ununuzi vimeongezeka kutoka 42 na 100 mwaka 2020/2021 hadi kufikia 43 na 109 mwaka 2024/2025 mtawalia.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Wizara imeyatambua na kuyapa hadhi ya vituo vya ununuzi jumla ya maeneo 142 yanayotumika kufanyia biashara ya madini kwa wingi (bulk minerals) kupitia Gazeti la Serikali Na. 906 ya tarehe 15 Novemba, 2024.
Akielezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, leo Mei 24, 2025 Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema kuwa mwaka 2017, Serikali ilisitisha minada ya ndani ya madini ya vito na maonesho ya madini kwa lengo la kutafuta namna bora ya uendeshaji.

Amesema kuwa Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini kwa kushirikiana na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) ilifanya mnada wa kwanza wa madini ya vito ndani ya nchi tarehe 14 Desemba, 2024 na mnada wa pili tarehe 8 Aprili, 2025 katika Mkoa wa kimadini wa Mirerani tangu kusitishwa mwaka 2017.
“Katika minada hiyo, jumla ya wanunuzi 60 walipatikana kama washindi wa mnada na kufanikiwa kununua madini yenye thamani ya shilingi 2,509,245,216.00 na kuwezesha Serikali kukusanya jumla ya shilingi 163,084,534.84 ikijumuisha mrabaha wa shilingi 149,218,787.80, ada ya ukaguzi ya shilingi 11,390,747.16, ada ya usimamizi wa mnada ya shilingi 2,509,245.22 na ada ya ushiriki wa mnada shilingi 6,850,852.50” amesema Mavunde.
Waziri Mavunde amesema kuwa Wizara kupitia Tume ya Madini inategemea kufanya minada na maonesho ya kitaifa katika mikoa ya kimadini ya Arusha, Mirerani, Mahenge, Ruvuma na Tanga.

Pia maonesho ya kimataifa yanatarajiwa kufanyika Zanzibar na katika Miji ya Dar es Salaam na Arusha.
Utekelezaji wa Mining Vision 2030.
Amesema uwa Wizara ya Madini inaendelea na utekelezaji wa Mining Vision 2030 Madini ni Maisha na Utajiri inayoweka matamanio ya kuwa na usimamizi thabiti wa rasilimali madini ili kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye uchumi wa Taifa; kuboresha maisha ya watanzania; na kutoa fursa kwa mtanzania yeyote wakiwemo wakina mama, vijana na wenye mahitaji maalum kujiongezea kipato na hatimaye kutajirika kupitia shughuli za madini.
Katika kufanikisha hili, mambo yafuatayo yamezingatiwa ikiwa ni maeneo makuu yanayounda misingi ya maono hayo: Upatikanaji wa taarifa za jiosayansi hususan taarifa za kina za jiofizikia (High Resolution Airborne Geophysical Survey) kutoka asilimia 16 ya sasa hadi kufikia angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2030; kuboresha mfumo wa kisheria na kitaasisi ili kuwa na usimamizi makini na uliowazi wa Sekta ya Madini; na kuiwezesha Sekta ya Madini kufungamana na sekta nyingine za kiuchumi hususan Sekta za Viwanda, Kilimo, Ujenzi, Fedha na nyingine zinazotoa huduma kwenye Sekta ya Madini.
“Maeneo mengine yanayozingatiwa katika Mining Vision 2030 ni pamoja na kuboresha shughuli za wachimbaji wadogo hususan urasimishaji wa shughuli zao, kuwezesha upatikanaji wa teknolojia za kisasa na rahisi, masoko ya madini, na upatikanaji wa mitaji; na usimamizi thabiti wa shughuli za utunzaji mazingira kwa kushirikiana na Taasisi nyingine ili shughuli za madini zisiwe na athari hasi kwenye mazingira.

Vilevile, Wizara kupitia STAMICO imeendelea kuimarisha huduma za uchorongaji kwa wachimbaji wadogo kwa kununua mitambo 15 ya uchorongaji.
“Mitambo hiyo itachangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa taarifa za kina za jiosayansi hususan kuthibitisha uwepo wa madini mbalimbali katika maeneo yanayomilikiwa na wachimbaji wadogo” amesema.