Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuizawadia Klabu ya Simba kiasi cha Dola Laki Moja za Kimarekani endapo itafanikiwa kutwaa ubingwa wa Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Dkt. Mwinyi ametoa ahadi hiyo alipokutana na kuzungumza na Viongozi pamoja na Wachezaji wa Klabu ya Simba katika Hoteli ya Madinat Al Bahr.

Rais Dkt. Mwinyi aliwatia moyo Wachezaji na kuwatakia kila la heri kuelekea mchezo wao wa Fainali utakaochezwa kesho katika Uwanja wa New Amaan Complex dhidi ya Timu ya RS Berkane kutoka Morocco, majira ya saa kumi jioni, ambapo yeye mwenyewe atakuwa Mgeni Rasmi.

Amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) zinaunga mkono juhudi za Klabu ya Simba zilizowezesha kufikia hatua ya Fainali na amewahimiza Wachezaji kucheza kwa kujiamini ili kutwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.

Aidha, Dkt. Mwinyi amewasihi Mashabiki wa soka kuiunga mkono Simba SC kwa moyo mmoja na kuishangilia kikamilifu ili kuwapa hamasa Wachezaji katika kutimiza ndoto ya kutwaa Kombe la Shirikisho.

Hii ni mara ya pili kwa Klabu ya Simba kucheza Fainali ya Michuano ya CAF, baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 1993 dhidi ya Klabu ya Stella Abidjan ya Ivory Coast. Katika mchezo huo, uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Mgeni Rasmi alikuwa Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi na Simba ilipoteza katika mchezo huo.