MAAFISA wa Ukraine wamesema mashambulizi ya Urusi nchini humo yamesababisha vifo vya watu 12 huku jeshi la taifa hilo likitangaza kuyadungua makombora 45 na droni 266 katika mashambulizi hayo.
Kituo cha huduma za dharura cha Ukraine kimeelezea mashambulizi hayo kuwa “usiku wa hofu” wakati Urusi ikiendelea na mashambulizi yake kwa siku ya pili mfululizo mjini Kiev na maeneo mengine ya Ukraine.
Kwa sasa rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameitolea mwito viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuongeza shinikizo kwa Urusi kuachana na mashambulizi yake dhidi ya Ukraine.
Mapambano haya yanatokea wakati pande hizo mbili zikiendeleza hatua za ubadilishanaji mkubwa wa wafungwa kuwahi kushuhudiwa tangu Mosow ilipoanzisha uvamizi wake Ukraine mwezi Februari mwaka 2022.
Hali hiyo pia imetokea wakati Marekani ikitumia ushawishi wake kutafuta makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyodumu kwa miaka mitatu kati ya mataifa hayo mawili.
