Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imesema Soko la Nyama Choma Vingunguti litatoa ajira 232, zikiwemo 15 za kudumu.
Mkuu wa Masoko katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Alex Buberwa alisema hayo wakati akitoa taarifa ya mradi huo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa wakati uzinduzi wa soko hilo.
“Soko hili limepangwa kuhudumia wafanyabiashara wadogo 232 wakiwemo wachoma nyama 25, mamalishe 56, wauza vinywaji 26, wauza maduka 42, matunda na mbogamboga 48, wauza vinywaji vya asili 15, vinywaji baridi 14 pamoja na watoa huduma ndogo za kifedha,” alisema Buberwa.
Alisema wafanyabiashara hao watahitaji usaidizi katika shughuli zao za kila siku, hali itakayosababisha kuongezeka kwa ajira nyingine nyingi kwa vijana hivyo kuboresha utoaji wa huduma ndani ya soko hilo.
Buberwa alisema soko hilo limejengwa kwa gharama ya Sh milioni 729.6 zilizotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.

Alisema zaidi ya Sh milioni 619 zimetumika kulipa wazabuni na mafundi waliotekeleza mradi huo kwa mfumo wa utekelezaji wa miradi kupitia mapato ya ndani.
Buberwa alisema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatarajia kuongeza mapato yake kwa zaidi ya Sh milioni 112 kila mwaka kupitia ushuru na kodi zitakazokusanywa kutoka kwa wafanyabiashara.
Wafanyabiashara waliopangwa kuanza shughuli zao katika soko hilo walisema litaboresha maisha yao na kuleta heshima katika kazi wanazozifanya.
“Sasa tuna mahali pa kudumu pa kufanyia biashara. Tumepewa mazingira salama na bora, jambo ambalo litatuongezea wateja,” alisema Amina Shomari.
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto alisema kuzinduliwa kwa soko hilo kumerejesha imani ya wananchi.
