Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Makundi Maalum imetaja vipaumbele vitano itakavyovitekeleza katika mwaka wa fedha 2025/2026, vikiwa na lengo la kuimarisha ustawi wa jamii, kukuza usawa wa kijinsia na kuleta maendeleo jumuishi kwa makundi yote ya kijamii.
Akizungumza bungeni leo Mei 27, 2025 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo, Waziri Dkt. Dorothy Gwajima amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kukuza ushiriki wa jamii katika kupanga na kujifunza kupitia Taasisi na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii lengo ni kuongeza uelewa wa wananchi juu ya umuhimu wa ustawi wa familia na maendeleo yao.
Vingine ni Kutambua, kuratibu na kuendeleza ustawi wa jamii – ikiwemo kupambana na vitendo vya ukatili, kuwawezesha wanawake kiuchumi na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa watoto, wazee na makundi maalumu katika ngazi ya msingi na Kuratibu na kuimarisha utoaji wa huduma za maendeleo ya jamii ikijumuisha kukuza usawa wa kijinsia, kutokomeza ukatili na kuweka mazingira bora ya malezi na ukuaji wa watoto.

Waziri Gwajima ametaja pia kipaumbele kingine kuwa ni Kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia hususani kwa wafanyabiashara wadogo na walimu wa taasisi za maendeleo ya jamii, ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu na huduma kwa jamii,Kuendeleza miundombinu ya Wizara kwa ajili ya utoaji bora wa huduma mfano ni ujenzi wa jengo la utawala katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, linalotarajiwa kugharimu Shilingi Bilioni 5.7 na ambalo hadi Aprili 2025 limekamilika kwa asilimia 70.
Aidha, Dkt. Gwajima alieleza kuwa Wizara inaendelea kuratibu utekelezaji wa Programu ya Kuondoa Vikwazo na Kuimarisha Usawa wa Kijinsia (GTAP) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, ambapo hadi sasa Shilingi Milioni 990.7 zimetumika katika utekelezaji wake, zikiwemo shughuli za kusambaza na kujenga uelewa wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Jinsia na Wanawake (2023).
Katika hotuba yake, Waziri Gwajima pia ameshukuru mashirika yasiyo ya kiserikali, ya dini, sekta binafsi, vikundi vya kijamii pamoja na vyombo vya habari kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha jitihada za Wizara. Baadhi ya mashirika hayo ni pamoja na World Vision, HelpAge Tanzania, Save the Children, WiLDAF, CAMFED, TGNP, MEWATA, Barrick, Bakhresa Group, na wengine wengi.