Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mtwara
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa chini (TAKUKURU) mkoani Mtwara imefanikisha kuokoa zaidi ya Sh milioni 79 fedha za wakulima wa korosho kutoka vyama mbalimbali ya msingi mkoani humo kwa msimu wa mwaka 2024/2025.
Akizungumza leo Mei 27, 2025 mkoani Mtwara, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mtwara, Elisante Mashauri amesema kiasi hicho cha fedha zaidi ya Sh milioni 79 ni za wakulima hao wa korosho walizokuwa wakidai katika msimu huo wa mwaka 2024/2025 zililipwa katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025.
Aidha, kutokana na elimu iliyotolewa kwa wananchi, wamejenga ujasiri na kuwawezesha kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na ubadhilifu wa fedha za wakulima wa korosho katika vyama vyao vya msingi (AMCOS).
‘’Taarifa ilifanyiwa kazi na kuwezesha wakulima hao kulipwa fedha zao hizo zaidi ya Sh milioni 79 walizokuwa wakidai katika vyama vya msingi, majalada saba ya uchunguzi yalifunguliwa na yapo katika hatua mbalimbali za uchunguzi,’’amesema Mashauri.
Aidha, kupitia programu ya Takukuru Rafiki, katika kijiji cha Nakopi kata ya napacho wilayani Nanyumbu taasisi hiyo ilitatua kero ya wakulima wa zao hilo kutokana na kutolipwa kwa wakati fedha zao Sh milioni 18.4 na viongozi hivyo kusababisha chama kupata hasara kwa kupoteza mazao ya wakulima katika sekta hiyo ya kilimo.
Katika hatua nyingine, katika kipindi hicho taasisi hiyo imefanya ufatiliaji wa rasilimali za umma kwa kukagua miradi mbalimbali kumi na tatu ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 7 katika sekta ya afya, miundombuni ya elimu ili kubaini viashiria vinavyoweza kusababisha upotevu wa rasilimali hizo.
Pia imepokea malalamiko mbalimbali 82 ambapo taarifa zilizohusu rushwa zilikuwa 44 na zisizohusu rushwa 38 huku mikakati ya Aprili hadi Juni mwaka huu ni kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi mkuu, sifa za kiongozi anayestahili kuchaguliwa na madhara ya rushwa kwenye uchaguzi.
