Umoja wa Mataifa umesema kwamba unalazimika kupunguza kwa kiasi kikubwa mipango yake ya misaada ya kibinadamu duniani kote kutokana na kukatwa kwa ufadhili.
Umoja wa Mataifa umesema kwamba unalazimika kupunguza kwa kiasi kikubwa mipango yake ya misaada ya kibinadamu duniani kote kutokana na kukatwa kwa ufadhili uliochochea mamilioni ya watu kukabiliwa na hali mbaya.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kiutu OCHA ilisema kuwa inatafuta ufadhili wa dola bilioni 29 kwa mwaka wa 2025 ikilinganishwa na dola bilioni 44 zilizoombwa hapo awali mwezi Desemba.
Shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limesema kwamba litalazimika kufuta ajira zipatazo 3,500, na kupunguza asilimia 30 ya gharama za wafanyakazi wake.
Tangu kurejea madarakani kwa Rais Donald Trump, Marekani iliyo mfadhili mkuu duniani imepunguza kwa kiasi kikubwa misaada ya kigeni, na kuleta athari katika sekta ya misaada ya kiutu duniani kote.
Kupunguzwa kwa ufadhili wa Marekani kumekuwa na madhara makubwa kwa misaada ya dharura , kampeni za chanjo na usambazaji wa dawa za HIV.
