Taasisi ya kudhibiti dawa ya Marekani imeidhinisha dawa mpya ya kuzuia virusi vya Ukimwi.

Dawa hiyo inayofanya kazi kwa muda mrefu, Lenacapavir, inahitaji tu kutumika mara moja kila baada ya miezi sita na mwenyekiti wa ugunduzi wake, Daniel O’Day amesema uamuzi wa uongozi wa taasisi ya Chakula na Dawa wa kihistoria katika mapambano dhidi ya VVU.

Idhini hiyo inakuja huku utawala wa Rais Trump ukipunguza kufadhili mipango ya afya ya kimataifa ambayo ingesambaza dawa ya Lenacapavir katika nchi zenye kipato cha chini.

Lenacapavir, inayouzwa kupitia chapa ya Yeztugo, imeonyesha kupunguza hatari ya maambukizi ya VVU kwa zaidi ya asilimia 99.9 kwa watu wazima na vijana — hali inayofanya utendaji wake kuwa sawa na chanjo yenye nguvu.

Uwezo wa dawa hiyo ulifanyiwa majaribio makubwa mara mbili. Ya kwanza, iliyohusisha zaidi ya wanawake 2,000 barani Afrika hasa eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, ilisababisha kupungua kwa maambukizi kwa asilimia 100 na ilionyesha ubora zaidi ya kidonge cha kila siku cha Truvada.

Katika jaribio la pili, lililohusisha zaidi ya wanaume 2,000 na watu wa jinsia tofauti, ni maambukizo mawili tu yalirekodiwa – kiwango cha kinga cha asilimia 99.9, tena kuzidi Truvada.